Kinara wa upachikaji mabao wa mabingwa wa soka nchini Ujerumani FC Bayern Munich, kwa msimu huu,  Robert Lewandowski, amesema katu hatochoka kumshukuru aliyekua meneja wake kwenye klabu ya Borussia Dortmund, Jurgen Klopp ambaye kwa sasa yupo Anfield nchini England akikinoa kikosi cha Liverpool.

Lewandowski, amefichua siri hiyo alipohojiwa na muandishi wa habari wa jarida la FourFourTwo, kwa ajili ya kuelezea mafanikio yake ambayo kwa msimu huu yameonekana kupambana moto kutokana na kuwa kasi kubwa ya kupachika mabao tofauti na misimu iliyopita.

Lewandowski, amesema hana budi kumshukuru Klopp, kutokana na kumpa ujasiri wa kujiamini wakati wote na kujitambua yeye ni nani anapokua uwanjani.

Amesema meneja huyo ana sifa za kipekee, na alionyesha kumjali wakati wote walipokua Borussia Dortmund, kutokana na kutumia muda wake mwingi kumshauri na kumpatia mbinu za kiuchezaji.

Klopp, alimsajili Lewandowski kwenye klabu ya Borussia Dortmund mwaka 2010, akitokea nchini kwao Poland alipokua akiitumikia klabu ya Lech Poznan ambayo aliifungia mabao 32 katika michezo 52.

Akiwa na klabu hiyo ya Signal Iduna Park, kuanzia mwaka 2010-14, mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 27, alicheza michezo 187 na kufunga mabao 103.

Mwaka 2014, alijiunga na mabingwa wa soka nchini Ujerumani, FC Bayern Munich na amekua msaada mkubwa katika safu ya ushambuliaji ya klabu hiyo ambayo inanolewa na meneja kutoka nchini Hispania, Pep Guardiola.

Mpaka sasa akiwa na FC Bayern Munich, Lewandowski ameshacheza michezo 42 na kufanikiwa kufunga mabao 31, lakini tangu mwanzoni mwa msimu huu, amekua na kasi ya ajabu ya kupachika mabao.

Katika michezo kumi ya kwanza kwenye ligi ya nchini Ujerumani msimu huu, alifanikiwa kufunga mabao saba, kisha akafunga mabao matatu kati ya matano yaliyoipa ushindi FC Bayern Muncih wakati wa mchezo wa ligi ya mabingwa barani Ulaya dhidi ya Dinamo Zagreb, uliochezwa mwezi septemba.

Mwezi Oktoba alifunga mabao mawili kati ya matano yaliyoipa ushindi Bayern Munich, wakati wa mchezo wa ligi ya nchini Ujerumani dhidi ya Dortmund, na siku tano baadae alifunga mabao manne katika mchezo dhidi ya FC Köln.

Utafiti: Sababu Za Wanaume Wasio Na Fedha Kuwapenda Wanawake Wenye Maumbo Haya
Shilole Akiri Kufuatwa Na Wauza 'Unga'