Mshambuliaji kutoka nchini Ureno na klabu ya Real Madrid, Cristiano Ronaldo, amedai kuwa anajua ni kwa nini mpinzani wake kwa sasa ulimwenguni, Lionel Messi aliamua kupiga penati kwa kumpasia Luis Suarez wakati wa mchezo wa ligi ya nchini Hispania dhidi ya Celta Vigo majuma mawili yaliyopita.

Ronaldo alifumba fumbo hilo wakati wa mkutano na waandishi wa habari kuelekea mchezo wao wa mkondo wa kwanza wa ligi ya mabingwa barani Ulaya, uliowakutanisha na AS Roma huko nchini Italia.

“Najua kwanini alifanya hivyo, lakini sina cha ziada cha kuongeza,” alisema Ronaldo mwenye umri wa miaka 31 na kuwaacha wanahabari ‘kwenye mataa’ wakihangaika kujiuliza alichomaanisha.

Katika kutafuta alichomaanisha Ronaldo, baadhi waliona ni katika kuonyesha heshima kwa gwiji Johan Cruyff, ambaye alifanya tukio kama hilo enzi zake, wakati akiitumikia klabu ya Ajax mwaka 1982, huku mashabiki wengine wakidhani huenda Messi alikuwa akimsaidia Suarez kumkimbia Ronaldo katika mbio za kuwania tuzo ya mfungaji bora wa La Liga – Pichichi.

Pasi hiyo ya penalti katika mchezo ambao ulimalizika kwa FC Barcelona kuibuka na ushindi wa mabao 6-1, ilimfanya Suarez kukamilisha ‘hat-trick’ siku hiyo na kufikisha mabao 23 mbele ya Ronaldo aliyebaki na mabao 21 huku Lionel Messi akiwa na mabao 13.

Gerad Ajetovic Awasili Tanzania Kumabili Francis Cheka
TCAA yapata Mkurugenzi Mkuu Mpya