Jeshi la Wananchi Tanzania – JWTZ, limetoa siku saba kwa Wananchi kusalimisha mavazi ya kijeshi katika Vituo vya Polisi, ofisi za kata na katika kambi za Jeshi zilizokaribu yao na kukemea baadhi ya Taasisi ambazo zinawashonea watumishi wake mavazi mfanano na wa jeshi, huku likitoa ofa ya chai ya pamoja kwa watakaotii agizo hilo.
Akizungumza na waandishi wa habari hii leo Agosti 24, 2022 jijini Dodoma, Kaimu Mkurugenzi wa Habari na Uhusiano Makao makuu ya JWTZ, Luteni Kanali Gaudentius Ilonda amesema kwa ambaye hatowasilisha mavazi hayo kipindi kilichotolewa watachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria na taratibu zilizowekwa.
Amesema, “mavazi hayo ni pamoja na Kombati, Makoti, Tisheti, Suruali, Magauni, Kofia, Viatu, Mabegi na Kaptula zenye rangi zinazofanana au kushonwa katika Mtindo wa Jeshi na kifungu cha 178 cha sheria ya Kanuni ya Adhabu sura ya 16 na kifungu cha 6 cha sheria ya Majeshi ya ulinzi au yanayofanana nayo kinatoa maelekezo sahihi.”
Amesema, hatua hiyo inatokana na uwepo wa baadhi ambao hutumia mavazi hayo kuwatapeli Wananchi na wengine kufanya vitendo viovu ambao pia wamekuwa wakidhaniwa kuwa ni Wanajeshi na kwamba vitendo hivyo ni vya uvunjifu wa sheria za Nchi hivyo havipaswi kufumbiwa macho.