Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida), Geoffrey Tengeneza amesema ni ruksa kwa yeyote anayetaka kubadilisha kitambulisho chake cha Taifa kwa kulipia gharama ya Sh20,000.
Tengeneza ameyasema hayo kupitia mjadala wa Twitter Space, uliondaliwa na gazeti la Mwananchi ambapo amesema kuwa mwananchi yeyote mwenye nia hiyo atalazimika kufika kwenye ofisi yoyote ya Nida iliyo jirani kukamilisha taratibu ikiwemo kuongeza taarifa mpya zisizokuwepo kwenye kitambulisho chake cha awali.
“Mwananchi yeyote anaweza kwa hiari yake kuomba kitambulisho kipya kisicho na ukomo wa muda lakini anayeamua kufanya hivyo awe tayari kulipia gharama ya Sh20, 000,” amesema Tengeneza.
Aliyewahi huwa mbunge wa viti maalum- CHADEMA, Suzan Lyimo, a amesema mpango huo utawaondolea wananchi adha ya kulazimika kutafuta vitambulisho vipya kila ukomo wa muda unapofika huku wakitumia muda mrefu kutafuta vitambulisho badala ya kushiriki shughuli za uzalishaji.
“Hakukuwa na sababu za kuweka ukomo kwenye vitambulisho vya Taifa kwa sababu uraia ni suala lisilo na ukomo wa muda,” amesema Lyimo
Aidha, mdau William Shao amesema uamuzi huo una faida chanya na hasi kwa wananchi na Serikali yenyewe huku akitaja faida kuwa ni fursa ya kuingiza taarifa mpya kulingana na anuani ya makazi, umri, picha na mabadiliko ya teknolojia.