‘HamaHama’ iliyoshika kasi hivi karibuni ambayo inaonekana kuifaidisha zaidi CCM inayovuna kwa kasi kutoka kwa vyama vya upinzani imeibua tetesi kwa wabunge wengine machachari wa ngome ya upinzani kuwa mbioni.
Moto wa tetesi za wabunge hao kuwa mbioni kuhamia CCM ulikolezwa na mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema ambaye alidai kuna mbunge wa Chadema atakayetangaza kuhama kati ya Alhamisi na Ijumaa, akihusisha uamuzi huo na ‘kununuliwa’.
“Kati ya leo (Jumatano) na Ijumaa, pesa itakuwa na thamani kwa maisha ya mvulana mmoja ambaye ni mbunge kutoka Chadema,” aliandika Lema kwenye mtandao wa kijamii.
Wabunge ambao majina yao yako kwenye mjadala mzito kwenye mitandao ya kijamii wakihusishwa na hatua hiyo ni wale machachari wa Chadema, Saed Kubenea (Ubungo) na John Mnyika (Kibamba).
Mbali na wabunge hao machachari wa Chadema, mbunge wa Kaliua kwa tiketi ya CUF, Magdalena Sakaya naye ametajwa kuwa kati ya watakaotangaza kutimkia CCM wiki hii.
Hata hivyo, wabunge wote walipohojiwa wamekanusha vikali tetesi hizo wakisisitiza kuwa habari hizo hazina ukweli.
“Sio kweli, hizo ni habari za uongo,” Mnyika alijibu tetesi hizo kwa ufupi bila kutaka kutoa ufafanuzi zaidi. Kauli yake iliongezwa nguvu na Meya wa Ubungo, Boniface Jacob ambaye alisisitiza kuwa mbunge huyo ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu wa Chadema (Bara) ‘hang’oki Chadema’.
Lakini Jacob anapaswa kukumbuka kauli aliyowahi kuitoa marehemu Mawazo, Kamanda wa Chadema kuwa “mtu pekee unayepaswa kumuamini kwenye harakati za kisiasa ni ‘wewe’.
Kwa upande wa Kubenea, alisema anataka kuzungumza na vyombo vya habari kwa pamoja kupitia mkutano na waandishi kuhusu tetesi hizo, lakini baadae alizungumza na chombo kimoja na kueleza kuwa hawezi kufanya hivyo.
Naye mbunge wa Kaliua, Sakaya yeye alisisitiza kuwa anafahamika kwa misimamo hivyo hawezi kuacha msimamo wake na kuhamia CCM.
“Mimi ni mbunge nimekuwa napongeza inbapobidi na kukosoa inapolazimu. Hao wanaosema [wanahama] ili kumuunga mkono Rais sijui kama wamekwenda shule? Kwani ukiwa upinzani hauwezi?” Sakaya alihoji.
Hata hivyo, siasa ni mchezo wa aina yake unaotumia ulimi ambao hauna mfupa, hivyo kubadili mkao wa ulimi ni rahisi na yakatokea yasiyotegemewa. Lakini pia, ulimi unaweza kusimamia kile ilichokieleza awali.
Mfano mkubwa ni wakati wa tetesi za Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa kuhamia Chadema wakati wa mchakato wa uchaguzi mkuu.
Kwa tunaokumbuka, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alikana hata picha zilizokuwa zinamuonesha Lowassa akitoka kwenye kikao cha Kamati Kuu ya chama hicho, lakini alikuwa na sababu ya msingi aliyoeleza baadae.
Hali hiyo ilisaababisha msemo wa ‘kubadili gia angani’ aliousema Mbowe kupata umaarufu katika kipindi hicho.
Hivyo, tuendelee kuhesabu saa na dakika kushuhudia kitakachotokea ndani ya kipindi hiki, huenda ikaishia kuwa tetesi tu, au yakatimia yale ya Wahenga kuwa ‘lisemwalo lipo na kama halipo laja’.
Je, hawa nao watabadili gia angani?
Kama alivyowahi kusema Mbowe mwaka 2015, watu ndio mtaji kwenye siasa. Hivyo, kila mwenye chama chake anajitahidi kuongeza kila iwezekanavyo mtaji wake.
Chadema wamemvuna aliyekuwa Mbunge wa Singida Kaskazini, Lazaro Nyalandu na CCM wameendelea kuvuna wabunge na madiwani kutoka kambi ya upinzani.
Mbivu na Mbichi zitajulikana, Muda ndio dawa na subira ni daktari wa zamu.