Mizozo, janga la Uviko-19 na mabadiliko ya tabianchi vimekuwa na madhara makubwa kwa afya ya wanawake na watoto duniani na hivyo kupelekea kuchochea udororaji wa ustawi wa watoto, wanawake na vijana.
Hayo yamebainishwa katika Ripoti ya Umoja wa Mataifa iliyotolewa jijini Berlin, Ujerumani wakati wa mkutano wa viongozi kuhusu masuala ya afya (WHS2022), ikisema mambo hayo yamerejesha nyuma kipimo kikuu cha ustawi wa mtoto, na vigezo vya kufikia malengo ya maendeleo endelevu, SDGs.
“Tangu ripoti ya mwisho kuhusu ya maendeleo ya kila mama na kila mtoto mwaka 2020, vipimo kama vile ukosefu wa uhakika wa chakula, njaa, ndoa katika umri mdogo, hatari ya kupiga kipigo kutoka kwa mpenzi, msongo miongoni mwa vijana balehe, vimeongezeka,” imesema ripoti hiyo.
Mambo yanayotajwa kurudi nyuma, ni pamoja na utoaji wa chanjo huku takwimu zikionesha kuwa watoto milioni 25 hawakuwa wamepata chanjo au hawakupata chanjo kamili kwa mwaka 2021, idadi ambayo ni nyongeza ya watoto milioni 6 ikilinganishwa na ile ya mwaka 2019.
Mamilioni ya watoto walikosa masomo wakati wa janga la Uviko-19, wengine kwa zaidi ya mwaka mmoja,na asilimia 80 ya watoto katika nchi 104 na maeneo walishindwa kusoma kwa sababu shule zilifungwa huku watoto milioni 10.5 wakipoteza wazazi au walezi wao kutokana na ugonjwa wa Corona.
Mizozo mingi imeshamiri, na nchi sita zinazoongoza duniani kwa kuwa na idadi kubwa ya wakimbizi wa ndani ni Afghanistani, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Ethiopia, Sudan, Syria na Yemen, zikiwa ni nchi miongoni mwa mataifa 10 ambayo wananchi wake hawana uhakika wa chakula.