Vipigo katika familia na ukatili wa kijinsia unaofanywa na baadhi ya wanaume dhidi ya watoto na wake zao mkoani Njombe umetajwa kusababishwa na mabadiliko ya tabia nchi yanayosababisha wanawake kutembea mwendo mrefu kwenda kuteka maji pamoja na kuokota kuni.
Mabadiliko hayo ya tabia nchi pia yametajwa kuwa chanzo cha watoto na wanawake kubakwa pindi wanapo kuwa porini kwenye shughuli za kijamii ambako kumekuwa kikwazo kikubwa katika ustawi wa jamii.
Kwa kuona hilo shirika lisilo la kiserikali linalojishughulisha na masuala ya ushirikishwaji wa jamii katika miradi endelevu la community participatory in sustainable development organization [COPASDO] lililopo Nazareth mjini Njombe chini ya ufadhili wa mfuko wa wanawake [Women Fund Tanzania] limelazimika kuanza kutoa elimu ya kukabiliana na mabadiliko ya tabia ya nchi ili kuepukana na ukatili dhidi ya wanawake, wasichana na watoto kwa kuanza na kata ya yakobi ndani ya halmashauri ya mji wa Njombe.
Mkurugenzi mtendaji wa shirika hilo Nestory Mahenge anasema ili kukabiliana na vitendo hivyo vinavyofanywa na baadhi ya wanaume wameamua Kutoa elimu kwa wanawake katika vijiji vyote vya kata ya Yakobi wakianza na viongozi wa vijiji na kata pamoja na wanawake wanaoviwakilisha vikundi mbalimbali vya Kifedha.
“lengo kubwa ni kujenga kwanza uelewa kwa viongozi na hawa wamama waweze kutambua haki zao zinazokandamizwa kutokana na mabadiliko ya tabia ya nchi na hivyo hata viongozi waweze kutengeneza sera mbadala zitakazo weza kumkwamua huyu mwanamke aweze kuondokana na vitendo vya unyanyasaji vinavyotokana na mabadiliko ya tabia ya nchi”.
Afisa maendeleo ya jamii kata ya Yakobi bi Renatha Nguli amesema ukatili ambao umekuwa ukiripotiwa katika Ofisi za serikali ndani ya kata hiyo ni utelekezwaji wa familia na vipigo vinavyofanywa na wanaume licha ya wanawake wengi kuweka siri vitendo wanavyofanyiwa.
“Unakuta mtu amefikia hali mbaya ndio anakuja ofisini .. hii ni kwa kuwa watu wengi wamekuwa wasiri,mpaka wanapigwa huko lakini kurepoti ni mara chache kuliko hizi za kutelekeza”alisema afisa maendeleo
Aida ngewe ni mkazi wa Kijiji Cha Idunda anasema sababu za wanawake kukaa kimya baada ya kufanyiwa ukatili ni kutokana na madhara yanayoweza kujitokeza baada ya sauti wanazoweza kupaza huku afisa mtendaji wa kijiji cha limage Bosco Mwenda akisema kuwa ujio wa shirika hilo na kuwapa elimu wanaamini itakwenda kupunguza kwa kiasi kikubwa vitendo vya ukatili pamoja na kuwataka wanaume kuachana na Kuwanyanyasa wanawake.