Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (Tantrade), Latifa Khamis amesema kampuni 3,200 zimethibitisha kushiriki Maonesho ya 46 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam yanayoanza leo kwenye Viwanja vya Sabasaba, Barabara ya Kilwa, Dar es Salaam.
Amesema hayo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari baada ya ufunguzi wa usafiri wa abiria wa mabasi ya mwendokasi kutoka Mbagala Rangi Tatu hadi katika viwanja hivyo.
Amesema kampuni 1,800 kutoka nchi 22 na 1,400 za Tanzania zimethibitisha kushiriki maonesho hayo. Kwa ushiriki kutoka nje, amesema Misri inaongoza kwa kusajili kampuni 65, ikifuatiwa na China yenye kampuni 22 na Pakistan kampuni 12.
Hata hivyo Latifa, amesema nchi nyingine zina kampuni hapa nchini lakini pia zimeleta kampuni zao na washiriki wao kutoka nje.
“Mwaka huu mwitikio ni mkubwa ikilinganishwa na miaka miwili iliyopita, hii yote inatokana na Rais Samia Suluhu Hassan kuimarisha diplomasia ya uchumi na kuutangaza utalii kimataifa kupitia filamu ya Royal Tour ambayo imewavutia wafanyabiashara kushiriki maonesho mwaka huu na ili wajionee hali halisi iliyopo nchini,”.