Kiungo mpya wa klabu ya Antalyaspor ya nchini Uturuki Samir Nasri, ametoa neno la shukurani kwa uongozi, wachezaji na mashabiki wa klabu ya Man City, mara baada ya kukamilisha uhamisho wake hapo jana.

Nasri aliyecheza kwa mkopo Sevilla CF msimu uliopita, ameondoka Man city moja kwa moja kwa ada ambayo imefanywa siri, kutokana na makubaliano yaliyofikiwa.

Kiungo huyo kutoka nchini Ufaransa alitoa neno la shukurani kwa uongozi, wachezaji na mashabiki wa Man City kupitia kurasa zake za mitandao ya kijamii.

“Ukurasa wa maisha yangu na Man City umefikia mwisho. Ninawashukuru viongozi na mashabiki wa Man City kwa ushirikiano walionionyesha nikiwa Etihad Stadium. Ahsanteni sana.

“Pia shukurani zangu ninaziwasilisha kwa wachezaji wa Man City ambao nilifanya nao kazi kwa ukaribu mkubwa hadi kufikia malengo yaliyokusudiwa klabuni hapo. Juhudi zetu kwa pamoja zilituwezesha kutwaa ubingwa wa ligi ya England mara mbili na ngao ya jamii. Shukurani nyingine nazituma kwa benchi zima la ufundi.

Samir Nasri alijiunga na Man city mwaka 2011 akitokea Arsenal, na mpaka anaondoka Etihad Stadium kwa mkopo msimu uliopita alikua amecheza michezo 124 na kufunga mabao 18.

Akiwa Sevilla CF katika msimu wa 2016/17 alicheza michezo 23 na kufunga mabao mawili.

Hili ni jibu la Ali Kiba kwa ‘Diss’ ya Diamond? ‘Najua unanichukia…’
Benzema Kubaki Real Madrid Hadi 2021