Mshambuliaji, Alexis Sanchez amesema kuwa hajutii kujiunga na klabu ya Manchester United licha ya kutopata muda wa kutosha wa kucheza na kuonyesha makali yake.
Sanchez amesema kuwa alikuwa mwenye furaha akiwa na Manchester United lakini alikuwa akiwashirikisha rafiki zake kwenye masuala yake ya uwanjani ambapo aliwaeleza kuwa anataka kucheza na endapo akiruhusiwa kucheza atafanya kila awezalo ila kilichomshangaza muda aliopewa ni kucheza dakika 60 kisha mechi inayofuata hachezi bila ya yeye kujua sababu ni nini.
Mchezaji huyo raia wa Chile, 30, amejiunga kwa mkopo na miamba ya soka nchini Italia klabu ya Inter Milan baada ya kudumu Old Trafford kwa miezi 19.
Sanchez alikuwa akilipwa mshahara mkubwa zaidi United wa pauni 400,000 kwa wiki lakini amefunga magoli matano katika mechi 45 alizoichezea United toka alipoihama Arsenal Juanuari 2018.
“Nilipojiunga Arsenal ilikuwa ni jambo kubwa na zuri nilikuwa mwenye furaha pale Arsenal lakini United ilikuwa ikitanuka, walikuwa wananua wachezaji ili kushinda kitu nilitaka kujiunga nao ili nami nishinde kila kitu.”amesema Sanchez.
Sanchez alipachika magoli 80 katika mechi 166 alizoichezea Arsenal ambao walimsajili kutoka Barcelona kwa pauni milioni 30 Julai 2014.
Baada ya mchezaji huyo kutua United aliandamwa na majeruhi na kuporomoka kwa kiwango chake ambapo alifunga magoli mawili katika mechi 27 za ligi alizocheza msimu uliopita japo aling’ara na timu ya taifa ya Chile kwenye kombe la Copa America akipachika magoli mawili kwenye mchezo wa nusu fainali.
Sanchez alianza kwenye michezo 31, kati ya 77 kwa United, na alimaliza michezo 13 tu.
Kabla ya kujiunga na Inter Milan, Sanchez hakucheza hata mchezo mmoja wa kirafiki wa kabla ya msimu na hakuwemo kwenye kikosi cha kocha Ole Gunnar Solskjaer kwenye michezo mitatu ya mwanzo huku klabu ikisema alikuwa majeruhi baada ya kuumia akiwa na timu ya taifa.
mchezaji huyo alisema alikuwa tayari kutumikia klabu yake baada tu ya Copa America.