Beki wa kulia wa klabu bingwa nchini Ufaransa Paris St Germain Serge Aurier, amehukumiwa kwenda jela kwa muda wa miezi miwili baada ya mahakama kumkuta na hatia ya kuwatolea lugha chafu askari.

Aurier mwenye umri wa miaka 23, alikuwa anakabiliwa na kesi hiyo ambayo chanzo chake kilitokea Mei 30 mwaka huu, alipotoa lugha chafu dhidi ya askari polisi waliokua nje ya klabu za usiku mjini Paris.

Mbali na kuhukumiwa kifungo, beki huyo kutoka nchini Ivory Coast pia ametozwa faini ya Euro 600 sawa na Pauni 520.

Hata hivyo Aurier amepinga hukumu iliyotolewa dhidi yake na ameahidi kukata rufaa, jambo ambalo linaendelea kumuweka uraiani hadi hapo shauri lake la kukata rufaa litakaposikilizwa na kutolewa hukumu.

Aurier anatarajiwa kuwa sehemu ya kikosi cha PSG ambacho siku ya jumatano kitacheza mchezo mzunguuko wa pili wa hatua ya makundi wa ligi ya mabingwa barani Ulaya dhidi ya Ludogorets.

Majuma mawili yaliyopita alicheza mchezo wa mzunguuko wa kwanza wa hatua ya makundi ya michuano hiyo, na alisaidia kupatikana kwa bao la mapema lililofungwa na mshambuliaji kutoka nchini Uruguay Edinson Cavani.

Spurs Yaenda Urusi, Yaacha Watano London
Aunty Ezekiel ajibu mashumbulizi ya mashabiki wake wanaosema anajipendekeza kwa Zari