Kutokana na ardhi kuwa ni urithi wa rasilimali na utajiri Serikali imesema inaweza kuandaa utaratibu wa kuwawezesha wananchi wamiliki kukodisha ama kuingia ubia na wawekezaji ili kuweza kunufaika zaidi.
Kauli hiyo imetolewa na Makamu Mwenyekiti wa Chama cha ACT – Wazalendo ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Othman Masoud Othman, kwa nyakati tofauti akiwa Mkoa wa Kaskazini Unguja alipokuwa kwenye ziara ya kichama katika majimbo tofauti ya uchaguzi mkoani huo.
Amesema, utaratibu wa serikali unaruhusu wananchi ama serikali kuingia ubia na wafanyabiashara au wawekezaji na wakaweza kunufakika na matumzi tofauti ya ardhi wanazomiliki kwenye maeneo yao kwa kukusanyaji kodi na mapato yatokanayo na rasilimali hiyo.
Ameongeza kuwa, sekta hiyo imekuwa haiwanufaishi wananchi kwa kutokuwepo kwa utaratibu bora unaowawezesha na kuwaelekeza wamiliki rasilimali hiyo kuwa na uwezo wa kuikodisha ama kuingia ubia na kuwa na maslahi nayo zaidi.
Akizungumzia matumizi ya rasilimali hiyo kwa kilimo, amesema mpango wa serikali ulipo hivi sasa ni kutumia ujuzi na maarifa ya wataalamu wa ndani ili kuitumia ardhi katika uzalishaji wa mazao na bidhaa mbali mbali za kilimo yakiwemo matunda.
Kwa upande wake Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama hicho, Ismail Jussa Ladhu, amewataka wananchi hasa vijana kutokata tamaa na kuendelea kushirikiana katika kuleta mabadiliko ya kidemokrasia nchini Zanzibar.