Na Lilian Mahena 

Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia  Dkt. Leonard Akwilapo amesema kuwa Wizara hiyo itakipatia Chuo Cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere Shilingi Milioni 500 kwa ajili ya ujenzi wa hosteli za wanafunzi katika Kampasi ya Karume, Zanzibar.

Dkt. Akwilapo ameyasema hayo alipofanya ziara ya kikazi katika  Kampasi ya Karume- Zanzibar, jana (Julai 31, 2019),  ambapo pamoja na mambo mengine amekagua maeneo ya chuo na kufanya kikao na wafanyakazi wa Kampasi hiyo.

Dkt. Akwilapo amesema  Wizara inatambua umuhimu wa elimu na ndio maana inajitahidi kwenda na kasi na kauli mbiu ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt. John Pombe Magufuli ya “Hapa kazi tu.”

“Nisisitize tu kuwa fedha kwa ajili ya ujenzi zitatolewa  mapema kwa Chuo ili kuunga mkono jitihada za Chuo za kutumia mapato yake ya ndani kwa kujenga Miundombinu ya kutolea elimu bora kwa wanafunzi” Alisisitiza Dkt. Akwilapo.

Dkt Akwilapo amesema Wizara ya elimu inafanya kazi kubwa katika kuendeleza falsafa ya Baba wa Taifa ya kufuta ujinga, umaskini na maradhi, na katika kuunga mkono jitihada za Chuo, Wizara itasaidia ujenzi wa hosteli za wanafunzi ili zianze kujengwa haraka kwa lengo la kutatua  changamoto ya makazi kwa wanafunzi.

Katibu Mkuu huyo pia amewapongeza wafanyakazi wa Kampasi ya Zanzibar kwa kufanya kazi kwa weledi na kuhakikisha Chuo kinajulikana na kuaminika kwa wakazi wa Zanzibar amba wamewapeleka watoto wao kusoka katika chuo hicho.

Katibu Mkuu Wizara ya Elimu,Sayansi na Teknolojia Dkt. Leonard Akwilapo akiwa katika picha ya pamoja na Menejimenti ya Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere Karume Kampasi Zanzibar

Awali akiwasilisha taarifa ya Chuo, Mkuu wa Chuo hicho, Prof.Shadrack Mwakalila amesema  kuwa Kampasi ya Karume inakuwa  kwa kasi  tangu kuanzishwa kwake, na kuwa   idadi ya wanafunzi wanaodahiliwa imeongezeka siku hadi siku kutoka wanafunzi 22 hadi kufikia zaidi ya wanafunzi elfu moja.

Aidha, Prof. Mwakalila alibainisha baadhi ya changamoto zinazoikabili Kampasi hiyo ya Karume iliyopo Zanzibar kuwa ni kukosekana kwa hosteli za wanafunzi, uvamizi wa maeneo ya Chuo na upungufu wa wafanyakazi.

Naye  Mkuu wa Kampasi ya Karume Zanzibar Dkt. Rose Mbwete ameahidi kuwa Chuo kitashirikiana vizuri na mamlaka zote husika katika kuhakikisha kinatekeleza majukumu yake vyema kwenye Jamii ili  kuinua viwango vya elimu nchini.

LIVE DAR ES SALAAM: Rais Magufuli katika ufunguzi wa Jengo Jipya la tatu la abiria Uwanja wa Ndege wa Kimataifa
LIVE DAR ES SALAAM: Rais Magufuli akizindua kiwanda cha kusaga Nafaka, Ngano na Mahindi