Familia ya aliyekuwa Mkurugenzi msaidizi wa Fedha za nje kutoka Wizara ya Fedha na Mipango, Mhandisi Leopold Lwajabe imethibitisha kuutambua mwili wa ndugu yao huyo licha ya kuukuta ukiwa na mavazi tofauti na aliyokuwa amevaa siku ya kupotea.

Mhandisi Lwajabe inadaiwa kwa mara ya kwanza alitoweka Julai 16 na kisha kupatikana, kabla ya baadaye tena kutoweka Julai 25 na hatimaye siku ya Julai 29, mwili wake ulikutwa ukiwa umening’inia juu ya mwembe Wilayani Mkuranga mkoani Pwani.

Msemaji wa familia hiyo, Mugisha Burrasio amesema kuwa familia imejiridhisha kuwa mwili huo ni wa ndugu yao waliyekuwa wanamtafuta.

”Siku hiyo alienda ofisini akiwa amevaa suruali nyeusi, viatu vyeusi na shati jeupe lakini tulivyokwenda kumuona mochwari tumekuta amevaa viatu na suruali zilezile, lakini tumekuta amevaa t-shirt ya bluu yenye michirizi ya kulala myeupe. Tshirt inaonekana mpya na marehemu hakuwahi kuwa na nguo ya namna hiyo katika historia ya maisha yake”, amesema Burrasio.

Aidha, Ibada ya kuaga mwili wa Mhandisi huyo itafanyika siku ya Alhamisi kinyerezi mwisho na mazishi yanatarajiwa kufanyika siku ya Jumamosi ya Agosti 3, 2019, Wilayani Karagwe mkoani Kagera. Marehemu ameacha mtoto mmoja wa kike.

Habari kubwa katika Magazeti ya Tanzania leo Agosti1, 2019
Sudan: Mauaji ya wanafunzi yapelekea shule kufungwa nchi nzima