Serikali nchini, imesema itahakikisha inaweka utaratibu mzuri wa sera, sheria na mifumo madhubuti ili kuwa na Mazingira rafiki ya uwekezaji katika Sekta ya Nishati na kuwataka Wadau wa maendeleo kuitumia vizuri fursa hiyo muhimu ili kufanikisha azma ya kumtua mama mzigo wa kuni kichwani.
Hayo yamebainishwa na Waziri wa Nishati, Januari Makamba wakati akihitimisha mjadala wa Kitaifa wa Nishati safi ya kupikia uliofanyika kwa sikumbili jijini Dar es salaam na kusisitiza umuhimu wa kila Mwananchi kuja na mawazo yatakayo liondoa Taifa katika tatizo la utumiaji wa Nishati chafu na kwenda kwenye Nishati safi.
Amesema “Huu ni wakati sahihi wa matumizi rasmi ya Nishati safi ya kupikia, na kama tulivyo msikia Rais wetu Mama Samia amesema tufanye kazi, na rais akisema hilo ni agizo hivyo nasi tutalitekeleza kwa kuangalia mambo yote yakliyo muhimu ili kufanikisha azma hii njema iliyokusudiwa.”
Mjadala huo wa Kitaifa wa Nishati safi ya kupikia, umefanyika kwa siku mbili (Novemba 1 – 2, 2022), na ulifunguliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ambaye ameitaka Wizara ya Nishati kufuatilia na kuhakikisha taasisi zote kubwa zianze kutumia nishati safi ya kupikia.