Serikali imesema kuwa ushauri wa Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe kuitaka iiburuze mahakamani Benki ya Standard ya Uingereza pamoja na watu waliohusika kwenye sakata la Escrow una mashiko na itaufanyia kazi.

Akiongea Bungeni hivi karibuni, Zitto aliitaka Serikali kuishtaki Benki hiyo badala ya kuwang’ang’ania madalali pekee (Harry Kitilya na Shose Sinare) wakati wapo waliotoa na kupokea rushwa katika uuzwaji wa hati fungani za Serikali zilizowezesha mkopo wa shilingi trilioni 1.2 kupitia Benki ya Stanbic tawi la Dar es Salaam.

Katika hatua nyingine, Zitto aliitaka Takukuru kuchunguza na kuwafikisha mahakamani watu waliohusika na sakata la Escrow huku akisisitiza kuwa bado kiasi kikubwa cha fedha kinalipwa kila mwaka kwa makampuni ya IPTL/PAP kama gharama za mitambo hata kama hawazalishi.

Akiongea na waandishi wa habari jana mjini Dodoma, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alisema kuwa Serikali imeupokea ushauri huo na itaanza kuufanyia kazi.

“Sisi kama Serikali tutaifanyia kazi na pale tutakapoona tumefikia katika hatua ya kutoa taarifa kwa umma kuhusu utekelezaji wa ushauri huo, tutafanya hivyo,” alisema Waziri Mkuu.

 

Uganda, Tanzania wapeana neema nyingine ya gesi
Picha: Amuua mpenzi wake na kuendelea kufanya mapenzi na ‘maiti yake’