Serikali imeanisha mikakati, sera na vipaumbele mbalimbali vinavyolenga katika kuhamasisha uhifadhi na utunzanji wa mazingira ikiwemo kuanzia kampeni za upandaji miti, kutokana na ukweli kuwa hakuna mbadala wa mazingira katika mustakabali wa maisha ya binadamu na viumbe hai.
Hayo yamebainishwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Dkt. Selemani Jafo katika uzinduzi wa Wiki ya Maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani leo (Juni
Mosi, 2023) Jijini Dodoma.
Amesema, kila mwanadamu anahitaji mazingira safi na salama, hivyo kutokana na umuhimu huo katika kutekeleza kwa vitendo kauli mbiu ya kilele cha maadhimisho ya siku ya mazingira duniani mwaka 2023, Serikali imekuja na ajenda mahsusi kwa wananchi kwa kupanda miti na usafi wa mazingira katika maeneo nchini.
“Sote ni mashahidi kuwa hivi karibuni tumeshuhudia mvua zisizo na wastani mzuri zikinyesha
katika baadhi ya maeneo ambazo zilileta athari ikiwemo vifo. Pia tumeshuhudia ukame mkali
katika Wilaya za Simanjiro, Longido na Kiteto hali iliyosababisha vifo vingi vya wanyama na
kusababisha hali ya umaskini wa kipato kwa wafugaji,” amesema Dkt. Jafo.