Serikali imesema kuwa kampeni ya kupambana na mashoga iliyotangazwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda pamoja na kauli alizozitoa kuhusu kampeni hiyo ni mawazo yake binafsi na kwamba sio msimamo wa Serikali.

Kupitia barua ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Serikali imesema kuwa itaendelea kuheshimu mikataba ya kimataifa ambayo imeisaini na kuiridhia.

“Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ingependa kufafanua kuwa hayo ni mawazo yake na sio msimamo wa Serikali,” imeeleza barua hiyo ambayo imewekwa kwenye tovuti ya wizara hiyo.

“Aidha, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ingependa kukumbusha na kusisitiza kwamba itaendelea kuheshimu mikataba yote ya kimataifa inayohusu haki za binadamu ambayo imesaini na kuridhia,” imeongeza.

Mkuu huyo wa Mkoa alitangaza wiki hii kuanza kampeni ya kudhibiti ushoga katika mkoa huo, akitaka watu wanaowafahamu mashoga kumtumia majina yao kwa namba ya simu iliyotolewa.

Alisema kuwa ataunda tume maalum ambayo itashughulikia suala hilo ikiwa ni pamoja na kuwapima watu hao.

Habari kubwa katika magazeti ya Tanzania leo Novemba 5, 2018
Vyuma vya reli (SGR) vilivyoibwa vyakutwa kwa Diwani