Mkuu wa Wilaya ya Tunduru, Julius Mtatiro amewataka Watanzania wenye mapenzi mema kumsaidia Mwalimu wa shule ya msingi Wenje iliyopo kata ya Nalasi wilaya humo Judith Chawe(29), aliyejifungua watoto wanne, ili aweze kuwatunza.
Mtatiro ameyasema hayo, baada ya kufika nyumbani kwa Mwalimu huyo ili kumjulia hali na kuwaona watoto hao, ambao amesema wanahitaji msaada na huduma ya karibu kwa sababu maziwa ya mama peke yake hayatoshelezi kuwahudumia watoto wote wanne.
Amesema, Serikali itakuwa jirani na Mwalimu huyo ili kujua maendeleo ya afya zao, huku akimuagiza Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Tunduru, Ombeni Hingi kumpatia huduma ya gari Mwalimu huyo kila atakapohitaji kwenda Hospitali kwa ajili ya uchunguzi wa afya yake na watoto.
“Kazi ya malezi ya watoto wanne ni kubwa kwa hiyo lazima Serikali na jamii imsaidie Mwalimu Judith katika malezi na maendeleo ya watoto ili wakue vizuri na kuwa na afya njema,” amesema Mkuu huyo wa Wilaya.
Awali, akiongea mbele ya ugeni huo, Mwalimu Judith amesema watoto hao wa jinsia ya kiume wawili na wa kike wawili alijifungua kwa njia ya kawaida katika Hospitali ya Misheni Mbesa ya Mkoani Ruvuma, na kwamba hali zao ni nzuri huku akibainisha kuwa huo ni uzazi wake wa pili na kuomba msaada wa vitu mbalimbali ikiwemo maziwa.
“Namshukuru sana Mungu kwa kuniwezesha kujifungua salama,vlakini kutokana na mahitaji makubwa ya watoto, nawaomba wasamaria wema wanisaidie mahitaji mbalimbali kama fedha na maziwa ili niweze kuwalea hawa watoto,”amefafanua Mwalimu Chawe.
Baba mzazi wa watoto hao, Hamis Shaibu amesema anamshukuru Mungu kwa kumwezesha kupata watoto wanne kwa mara moja, na kuiomba jamii iweze kuwasaidia kwa hali na mali mahitaji ya watoto hao.
Kwa upande wake Afisa Tarafa wa Nalasi, Salum Kijumu amesema baada ya kupata taarifa ya watoto hao wanne, watumishi wameanzisha utaratibu wa kumchangia fedha ili ziweze kumsaidia katika mahitaji yake muhimu.