Serikali nchini, imeamua kutoa kipaumbele cha juu kugharamia miradi ya maji ili itoe huduma endelevu ya majisafi na salama pamoja na elimu ya usafi wa mazingira kwa wananchi wote.
Hayo yamebainishwa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Philip Mpango hii leo Januari 19, 2023 mjini Shinyanga wakati akiweka Jiwe la Msingi Mradi wa Maji wa Ziwa Victoria utakaohudumia Tinde na Shelui na unaotarajia kugharimu shilingi bilioni 24.4.
Amesema, maji ni miongoni mwa Sekta za kipaumbele katika mkakati wa kukuza Uchumi wa Viwanda na kupambana na umaskini na kwamba kuboresha huduma hiyo kutapunguza muda wa kutafuta na kuchota maji, ili kuwawezesha Wananchi kufanya kazi za kimaendeleo.
Dkt. Mpango pia amesema hatua hiyo itasaidia kuongezeka kwa muda wa Wanafunzi kuhudhuria masomo, kuimarisha afya na kuepusha magonjwa yanayotokana na matumizi ya maji yasiyo safi na salama.