Serikali imewataka wanaonunua ardhi jijini Dar es Salaam kuhakikisha kabla ya kufikia hatua hiyo wanaonana na wataalam wa manispaa.
Akizungumza jana katika wilaya ya Kigamboni, eneo la Vijibweni, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi amesema kuwa mtu yoyote atakayenunua ardhi jijini humo bila kuonana kwanza na watalaam wa ardhi wa Manispaa husika ajiandae kisaikolojia kununua bomu.
Aidha, Waziri Lukuvi amewapiga marufuku viongozi wa Serikali za mitaa ambao wamekuwa wakitoa mikataba na hata hati za ardhi kwa watu mbalimbali kwa madai kuwa ni ‘hati za ardhi za serikali za mitaa’, kwani sheria haiwaruhusu kufanya hivyo.
“Kuna mahali nimeshuhudia, mwenyekiti wa mitaa anagonga mihuri mitatu kwenye kiwanja kimoja na wengine wameanza kutengeneza hati, wanaziita hati za ardhi za mitaa. Ni marufuku Serikali za mitaa kuwa na hati, hamruhusiwi kisheria,” alisema Waziri Lukuvi.
Waziri huyo aliyasema hayo alipokuwa akiwasikiliza wananchi wa Kijibweni ambao wamekuwa kwenye mgogoro wa ardhi na muwekezaji raia wa Korea ambaye alinunua ardhi kwa lengo la kujenga Chuo Kikuu katika eneo hilo, lakini licha ya Mahakama kutoa hukumu kuwa wananchi walipwe shilingi milioni moja kwa kila hekari kama fidia, wamedai ameendelea kuwalipa Sh 400,000 kwa hekari.