Serikali nchini, imetoa mwongozo kwa Halmashauri ambazo zinakabiliwa na njaa na kuhitaji chakula cha bei nafuu au msaada kwa wananchi wake ambapo Mkurugenzi wa Halmashauri husika kuandika barua kwa Waziri Mkuu kupitia Wizara ya Sera, Bunge na Uratibu yenye jukumu la kutoa kibali kwa wataalamu kujiridhisha kama kuna uhitaji wa chakula.

Mwongozo huo, umetolewa bungeni hii leo Februari 3, 2023 na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera na Bunge, George Simbachawene wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Viti Maalumu, Ferister Njawu ambaye alihoji ni mkakati gani ambao Serikali inachukua katika kuwasaidia watanzania katika maeneo mengi ambako wanakabiliwa na baa la njaa kwa sasa.

“Ofisi ya Waziri Mkuu ikishapokea taarifa hiyo, itaagiza wataalamu kutoka wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) ambao watakwenda kujiridhisha kama eneo hilo linahitaji chakula cha bei ndogo atatafutwa wakala na kama kunahitajika chakula cha bure taarifa itaeleza,”amesema Simbachawene.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera na Bunge, George Simbachawene akijibu swali la nyongeza la mbunge wa Viti Maalumu Ferister Njawu Bungeni  Dodoma leo Ijumaa, Februari 3, 2023. Picha na Said Khamis.

Mbunge wa Korogwe Vijijini, Timotheo Mzava (CCM) alihoji Serikali ina mpango gani wa kusaidia upatikanaji wa chakula cha bei nafuu kwa wananchi walioathirika na ukame wa chakula.

Ambapo Naibu Waziri wa Kilimo Anthony Mavunde alijibu Serikali kupitia NFRA imeendelea kutoa chakula na kukiuza chini ya bei ya soko ambapo ameeleza kuwa hadi Januari 31, 2023 kiasi cha tani 24,975.152 zimepelekwa na kuuzwa katika halmashauri 60 nchini katika vituo vya mauzo 116.

Kwa mujibu wa Naibu Waziri, eneo lingine lililopelekwa chakula cha bei nafuu ni Wilaya ya Iringa Vijijini ambako linapatikana Jimbo la Karenga alikosema mahindi yataanza kupelekwa kesho Februari 4, 2023.

Asimulia magumu ya kuganga njaa, haamini kama kapata kazi
Wahimizwa matumizi sahihi ya Takwimu za sensa kupanga maendeleo