Siku chache baada ya Serikali kupitia Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), kutangaza ajira za walimu 13,000 na kutokea kwa makosa mbalimbali kwenye mfumo, Katibu Mkuu OR TAMISEMI  Mhandisi Joseph Nyamhanga ametolea ufafanuzi wa baadhi ya mapungufu yaliyoonekana katika orodha ya walimu walioajiriwa.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma Mhandisi Nyamhanga amesema kuna baadhi ya makosa ya kimfumo yalijitokeza ikiwamo jina la mwalimu Abdallah Shonde ambaye jina lake limetokea kwenye kurasa 196, na kufafanua kuwa jina hilo lilitokea kimakosa, wakati wa kuweka kichwa cha habari ya kurasa husika.

“Jina hili lilitokea baada ya wakati ya kuweka kichwa cha habari ndipo hilo jina likatokea kimakosa kwenye mfumo lakini halijaongeza idadi wala kupunguza ajira za walimu wengine bali iliongeza namba ya wingi wa majina tu, lakini tulifanyia marekebisho siku ileile” amesema Mhandisi Nyamhanga.

Kuhusu kosa la pili la kimfumo ambalo lilikuwa ni mwalimu Benjamini Billal kupangiwa shule binafsi, Nyamhanga amebainisha kuwa serikali huingia makubaliano na shule binafsi na za dini za watu wenye mahitaji maalumu ya kusaidiana kwenye shule hizo zinazopokea wanafunzi wa mahitaji maalumu.

“Lakini kwa mwalimu huyu alipangiwa kimakosa kwenye shule ya Mwalimu Tuntube Kigoma na tayari tumembadilisha na sasa tumempangia shule ya Malagalasi huko huko Kibongo Kigoma, tumeona tusimpeleke mbali” amesema.

Aidha, Nyamhanga ameongeza kuwa mapungufu mengine  yalikuwa ni baadhi ya walimu ambao wanaonekena walimaliza kidato cha nne mwaka 2019, 2018 na 2017, suala ambalo amesema ni makosa ya waombaji wenyewe kwenye kujaza fomu, kwa sababu mfumo ulikuwa hauruhusu kufanya marekebisho.

“Tumejaribu kupitia majina ya walimu hao na tumebaini walimu hao walimaliza kidato cha nne kuanzia mwaka 2013 na kidato cha sita walimaliza mwaka 2016 na hakuna mwalimu aliyeajiriwa akiwa amemaliza kidato cha nne mwaka 2019 na 2018” amesema Mhandisi Nyamhanga.

Vilevile, amebainisha kuwa hakuna mwalimu aliyeajiriwa mwenye umri wa zaidi ya miaka 45 na kubainisha kuwa kuhusu mwalimu anayedaiwa kuajiriwa akiwa amemaliza chuo mwaka 1994,  uhakiki umebaini alizaliwa mwaka 1995 na alimaliza elimu ya cheti mwaka 2015.

Kwa upande wake Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Utumishi na Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt. Laurian Ndumbaro amesema makosa mengi yamejitokeza baada ya waombaji wengi kufanya makosa mengi kwenye uombaji.

Amesema ajira 13000 zinatolewa kwa awamu mbili ambapo kwa awamu ya kwanza wameajiri walimu 8000, na awamu ya pili wataajiri walimu 5000 kwa mwaka huu wa fedha 2020 hadi 2021, huku akitoa onyo kwa walimu waliogushi masomo ambayo hawakusomea kwa lengo la kupata kipaumbele kuwa wataondolewa kwenye mfumo moja kwa moja watakapobainika.

Habari kubwa kwenye magazeti leo, Desemba 1, 2020
Spika awaapisha Polepole, Lulida