Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Philip Mpango amesema Serikali za Afrika zinapaswa kuchukua hatua mbalimbali ikiwemo kuwapa wakulima wadogo pembejeo za bei nafuu, maarifa, ujuzi na mitaji ili kuongeza tija katika mnyororo wa thamani wa uzalishaji chakula.
Dkt. Mpango ametoa wito huo wakati akifungua Mkutano wa Jukwaa la Mifumo ya Chakula Barani Afrika kwa Mwaka 2023 (AGRF), unaofanyika jijini Dar es salaam na kudai kuwa pamoja na mambo mengine Afrika inahitaji kutumia maarifa yaliyopo ya kisayansi ikiwa ni pamoja na teknolojia ya kiasili, ili kuzalisha na kusindika chakula cha kutosha kwa ajili ya watu wake na masoko ya kimataifa.
Amesema, ni muhimu kuendelea kufadhili tafiti za kisayansi, matumizi ya dijitali, kutambua mchango wa wanawake na vijana katika kilimo, pamoja na kuwavutia vijana kwa kuongeza matumizi ya teknolojia ya kisasa, upatikanaji rahisi wa ardhi, mitaji na masoko yanayolenga shughuli kama vile kilimo cha bustani ambacho kina matokeo ya haraka zaidi.
Aidha, Dkt. Mpango pia ameongeza kuwa mageuzi katika mifumo ya chakula yanaenda sambamba na ukuaji wa sekta zingine ikiwemo usafirishaji wa bidhaa za chakula hivyo nchi za Afrika zinapaswa kuheshimu mipango ya biashara ya kikanda, hasa Mkataba wa Eneo Huru la Biashara Barani Afrika (AfCFTA), kwa kuzingatia itifaki za kibiashara na kuondoa vikwazo visivyo vya kiforodha.