Shahidi wa kesi dhidi ya mfanyabiashara bilionea wa dawa za kulevya, Joaquín “El Chapo” Guzmán, ameiambia Mahakama ya New York kuwa bilionea huyo alimhonga Rais wa zamani wa Mexico, Enrique Peña Nieto kiasi cha $100 milioni.
Shahidi huyo aliyetambulishwa kwa jina la Alex Cifuentes ambaye alikuwa mtu wa karibu na El Chapo, amedai kuwa alivieleza vyombo vya usalama kuhusu rushwa hiyo mwaka 2016, wakati huo Pena Nieto alikuwa Rais.
Peña Nieto alikuwa Rais wa Mexico tangu mwaka 2012 hadi 2018.
Kwa mujibu wa waandishi wa habari walioko ndani ya Mahakama hiyo iliyo eneo la Brooklyn, Peña Nieto aliomba apewe $250 milioni, lakini aliafiki kupunguza na kupokea $100 milioni ambazo ziliwasilishwa kwake na rafiki wa El Chapo.
Mhalifu huyo ambaye amewahi kutoroka katika jela zenye ulinzi mkali mara mbili, anashtakiwa kwa kuwa kiongozi wa mtandao mkubwa wa dawa za kulevya ambao unadaiwa kusambaza kiasi kikubwa cha dawa hizo nchini Marekani.
El Chapo mwenye umri wa miaka 61, amekuwa akikabiliwa na mashtaka hayo nchini Marekani tangu Novemba mwaka jana, aliposafirishwa kutoka Mexico kwa madai kuwa anamiliki mtandao mkubwa zaidi duniani wa dawa za kulevya.
Rais huyo wa zamani wa Mexico bado hajazungumzia tuhuma hizo tangu zifikishwe Mahakamani, lakini Novemba mwaka jana alizikanusha vikali zilipoanza kuenezwa.