Serikali ya Uganda inaupitia upya uamuzi wake wa kuweka kodi kwa matumizi ya mitandao ya kijamii ikiwa ni pamoja na Whatsapp na huduma za kutuma fedha kwa njia ya simu, kufuatia taharuki ya kuibuka maandamano.
Hatua hiyo imetangazwa na Waziri Mkuu, Ruhakana Rugunda muda mfupi baada ya jeshi la polisi kufanya jitihada za kuzuia maandamano yaliyokuwa yanalenga kupinga kodi hizo zinazowaongezea watumiaji gharama za matumizi ya mitandao ya kijamii na huduma za kifedha.
Rais Yoweri Museveni alisema kuwa uamuzi wa kuweka kodi kwenye vyanzo hivyo ni kuongeza pato la Serikali pamoja na kupunguza umbea kwenye WhatsaApp, Facebook na Twitter.
Wakosoaji wake wamedai kuwa lengo la Museveni ni kuwanyamazisha watu wanaomkosoa. Kwa mujibu wa sheria hiyo, watumiaji wa mitandao ya kijamii wanatakiwa kulipia kodi ya Sh200 za Uganda, sawa na $0.05.
Kadhalika, sheria hiyo imeweka kodi ya asilimia moja ya fedha zinazotumwa kupitia njia ya simu, hatua inayolalamikiwa kuwa inaongoza ugumu wa maisha kwa wananchi masikini ambao wanategemea zaidi huduma za simu kuliko benki.
Hata hivyo, baadhi ya watu wamekuwa wakitumia mfumo wA Virtual Private Networks (VPN) kukwepa kulipa kodi hiyo.
Awali, polisi waliwashikilia watu wawili na kuwatawanya kwa mabomu ya machozi watu waliokuwa wanataka kuandamana kupinga sheria hiyo.
Zaidi ya watu 300 walikusanyika wakiongozwa na Mbunge wa kujitegemea ambaye pia ni mwanamuziki, Robert Kyagulanyi maarufu kama Bobi Wine.
Kupitia Twitter, Bobi Wine ameweka ujumbe na picha inayoonesha mkusanyiko huo akiwashukuru waliofika huku akidai kuwa polisi walitaka kumkamata lakini walishindwa na nguvu ya umati uliokuwepo.
I would like to thank whoever came through and added a voice to the struggle against the unfair taxation. The police fought so hard to arrest me but the power of the people overpowered them…. pic.twitter.com/BCdxPocY7k
— BOBI WINE (@HEBobiwine) July 11, 2018