Mamlaka ya Maji safi na usafi wa Mazingira Morogoro – MORUWASA, kwa kushirikiana na Bodi ya Maji Bonde la Wami Ruvu na Manispaa ya Morogoro, wamefanya usafi katika chanzo cha maji Vituli kata ya Bingwa na kubaini uwepo wa baadhi ya watu kufanya shughuli za kibinadamu kwenye chanzo cha maji Mto mgolole.
Hali hiyo imebainika baada ya Mamlaka hizo kufika eneo hilo kutoa elimu kwa wananchi kuacha kutupa taka za plastiki katika vyanzo vya maji na kukuta baadhi yao wakifanya uharibifu huo.
Wakiwa eneo hilo, Afisa maendeleo ya jamii Bodi ya Maji Bonde la Wami Ruvu, Yuliani Mizola ametumia nafasi hiyo kutoa elimu kwa wananchi kutojenga vyoo karibu na chanzo cha mto kwani kunaweza kusababisha mlipuko wa magonjwa ikiwemo Kipindupindu.
Kwa upande wake msimazi wa mazingira MORUWASA, Mhandisi Rashid Bumalwa wamesema kutokana na uchafunzi huo wamekua wakitumia gharama kubwa kutibu maji hivyo mamlaka inawakumbusha wananchi kuendelea kutunza na kuhifadhi vyanzo vya maji.
Naye afisa mazingira Manispaa ya Morogoro, Fatma Juma amesema licha ya kufanya usafi katika vyanzo vya maji lakini wamekua wakitoa elimu kwa wananchi kufanya usafi hadi katika makazi yao na hivyo kutoa elimu zaidi kwa wakazi wanaoishi karibu na yanzo vya maji kwq kuona umuhimu wa vyanzo hivyo.
Amesema sheria ya Mazingira inakataza kufanya shughuli za kibinadamu ikiwemo kilimo, ufugaji, uchimbaji madini na ujenzi wa nyumba ndani ya mita sitini, kutoka kwenye chanzo cha maji.