Chama cha Wazazi na Watoto wenye Ulemavu wa Mtindio wa Ubongo, Akili na Viungo Tanzania (CHAWAUMAVITA) kinatarajia kufanya maadhimisho ya siku ya mtindio wa ubongo duniani jijini Dar es salaam kwa lengo la kuipa jamii uelewa juu ya changamoto wanazozipata.

Hayo yamesemwa leo Jijini Dar es Salaam na Mwenyekiti wa chama hicho, Hilali Said alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maadhimisho hayo.

Amesema kuwa nchi mbalimbali duniani huadhimisha siku hiyo kwa kutoa elimu ya ulemavu wa aina hiyo kwa wananchi ili kupunguza athari zinazojitokeza kwa wazazi na watoto wenyewe pamoja na kuwasaidia wanachama kutetea na kupata haki zao kwa mujibu wa sheria.

“Kwa kawaida Siku ya Mtindio wa Ubongo duniani huadhimishwa kila Jumatano ya kwanza ya mwezi Oktoba lakini kwa mwaka huu itaadhimishwa tarehe 6, ambapo yanategemewa kufanyika katika viwanja vya shule ya msingi Mjimwema vilivyopo Wilaya ya Kigamboni na tunategemea mgeni rasmi wa maadhimisho hayo  atakuwa Mkuu wa Wilaya hiyo Hashim Mgandilwa,”amesema Said

Aidha, ameongeza kuwa chama hicho kwa sasa kinafanya kazi Jijini Dar es Salaam pekee ambapo kuna jumla ya vituo kumi vinavyowasaidia watoto wenye matatizo hayo kupata huduma ya mazoezi ya viungo vilivyoathirika mara moja kwa wiki.

Hata hivyo, kwa upande wake mweka hazina wa chama hicho, Jane Kim ameiomba Serikali kuwasaidia watoto hao kwa kuwapatia mazingira mazuri ya kusomea pamoja na walimu wa kutosha wenye elimu stahiki ikiwa ni pamoja na kuwapatia ulinzi wa kutosha wanapokuwa shuleni ili nao waweze kupata elimu na kutimiza ndoto zao kama watoto wengine.

 

Tanzanite yarejea Dar kuivaa Nigeria
Ujerumani yaipatia Tanzania msaada wa bil. 521