Tanzania imepatiwa msaada wa kiasi cha Euro milioni 198.5 ambazo sawa na shilingi bilioni 520.86 za Kitanzania kutoka nchi ya Ujerumani zilizotumika kufadhili miradi mbalimbali ikiwemo ya Maliasili na Mazingira, Afya, Maji, Nishati, Udhibiti wa Fedha za Umma (Good Financial Governance) na Kusaidia huduma za Wakimbizi katika mkoa wa Kigoma, katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita.

Hayo yamesemwa Jijini Dar es Salaam na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Amina Khamis Shaaban wakati wa tukio la Tanzania na Ujerumani kusaini kumbukumbu za Mkutano wa Mashauriano ya Kimaendeleo (Bilateral Development Consultations) ambapo Ujerumani imeonyesha nia ya kuendelea kuisaidia Tanzania katika Sekta hizo kuanzia mwaka 2018 hadi 2021.

Aidha, mkutano huo ni maandalizi ya mkutano wa Majadiliano ya Kimaendeleo (Bilateral Negotiations) kati ya Tanzania na Ujerumani unaotarajiwa kufanyika mwaka 2018 ambapo Serikali ya Ujerumani itatangaza kiasi cha fedha watakazotoa kama msaada kwa ajili ya kufadhili Sekta zilizoainishwa.

“Tunaishukuru Ujerumani kwa kuwa miongoni mwa washirika wa muda mrefu wanaotoa misaada mikubwa ya kimaendeleo kwa Tanzania na sisi tunaahidi kuendeleza ushirikiano huo kwa faida ya pande zote mbili,” amesema Amina Shaaban.

Hata hivyo, kwa upande wake, George Rademacher kwa niaba ya Serikali ya Ujerumani amesema kuwa Tanzania imekuwa na sifa njema nchini Ujerumani hasa kwa sababu ya amani iliyopo, jinsi ambavyo imehifadhi maliasili zake na kuifanya kuwa nchi yenye vivutio vya kipekee vya utalii.

 

 

Siku ya mtindio wa ubongo kuadhimishwa jijini Dar
Video: Man Walter atoboa siri kuhusu 20% na Mr.Nice, aitaja 'Seduce me' ya Ali Kiba