Kiungo Mshambuliaji kutoka Tanzania Simon Msuva amefunguka usajili wa Mshindi mara Tano wa Ballon d’Or, Cristiano Ronaldo aliyejiunga na Klabu ya Al-Nassr FC.
Usajili wa Ronaldo umekua gumzo Duniani huku Mashabiki wa Klabu ya Al-Nassr FC wakionesha kufurahishwa na ujio wa Staa huyo, ambaye aliwahi kutamba na Klabu za Manchester United (England), Real Madrid (Hispania) na Juventus (Italia).
Msuva amesema usajili wa Ronaldo huko Saudi Arabia umeongeza chachu ya ushindani katika Ligi Kuu ya nchini humo na hata katika madaraja ya chini, ambako yeye anacheza akiwa na Klabu ya Al Qadsiah FC.
Amesema anaamini usajili wa Nyota huyo utaendelea kutoa nafasi kwa Mashabiki wengi Duniani kuifuatilia Ligi Kuu ya Saudi Arabia, na kuepelekea Nyota wengine wakubwa kutamani kucheza nchini humo.
“Ni jambo zuri kuona wachezaji wakubwa duniani kama yeye wakivutika na kuja huku, hiyo ina maana kuwa watu watakuwa wakitupia macho. Kwangu natazama hili kama fursa hivyo natakiwa kuongeza juhudi zaidi,” amesema Msuva.
Hata hivyo itamlazimu Msuva kusikilizia hadi msimu ujao kuona kama atapata Fursa ya kucheza dhidi ya Klabu ya Al-Nassr FC kwenye Ligi Kuu, endapo Klabu yake ya Al Qadsiah FC au Kombe la Mfalme ambapo timu za madaraja ya chini hushiriki.
Klabu ya Al Qadsiah FC lipo katika nafasi ya 13 kwenye msimamo wa timu 18 huku wakikusanya alama 16 kwenye michezo 14 ya Ligi Daraja la Kwanza (Saudi First Division League).