Nidhamu, bidii ya mazoezi na kujituma ndiyo sababu zilizotajwa kuchangia Bondia wa ngumi za kulipwa nchini Tanzania, Karim Mandonga kushinda mkanda wa ubingwa wa PST dhidi ya mpinzani wake, Kenneth Lukyamuzi wa Uganda.
Pambano hilo la Raundi nane uzito wa juu lililofanyika juzi Jumamosi (Machi 25) katika Ukumbi wa Kasarani, Nairobi nchini Kenya.
Kocha wa Mandonga, Said Kisopu amesema siri kubwa ya Bondia wake kushinda ni nidhamu ya mchezo na kuongeza bidii katika kufanya mazoezi.
Kocha huyo amesema katika mapambano matano mfululizo ambayo Mandonga amecheza amebadilika na kucheza kwa kiwango kikubwa tofauti na kipindi cha nyuma.
“Kujituma, nidhamu ndiyo kitu kikubwa kilichosababisha Mandonga kumshinda mpinzani wake,” amesema Kisopu.
“Tunashukuru katika mapambano matano yote ameshinda, pia tunahitaji kuweka heshima zaidi ndiyo maana akashinda mkanda nje ya nyumbani Tanzania,” amesema Kisopu.
Naye Promota wa pambano hilo, Meja Selemani Semunyu amesema baada ya kumaliza kwa pambano hilo anatarajia kuandaa mtanange mwingine siku ya Idd Pili, litakalofanyika mkiani Morogoro.
Amesema wadau wa ndondi nchini wategemee burudani za kutosha mwaka huu 2023, baada ya mfungo wa Ramadhani kutakuwa na pambano.
“Mwaka huu kuna mapambano mengi na mabondia wenye rekodi nzuri katika ngumi, wadau wa ngumi nawaomba waendelee kunisapoti kwa sababu Aprili mwaka huu kuna burudani nzuri inakuja,” amesema Semunyu.
Pamoja Mandonga kushinda mabondia wengine ambao waliibuka kidedea katika mkanda wa PST ni Hassan Ndonga alimchakaza kwa pointi Mkenya, Nick Otieno, Fatuma Yazidu alimtwanga, Consalata Musanga kutoka Kenya huku Zawadi Kutaka na George Mbonabucha wakipoteza.
Zawadi alicheza na Plaxedus Odouri wakati Mbonabucha alipoteza kwa Albert Kimario wote kutoka Kenya.