Balozi Willibrod Slaa ameunga mkono uwekezaji kwenye Bandari ya Dar es Salaam, lakini ameishauri Serikali kurekebisha kasoro zinazolalamikiwa kwenye mkataba wa uwekezaji na kampuni ya DP World ya Dubai.
Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, Slaa amesema kuwa mikataba ya nchi hodhi (host government agreement) na mikataba kati ya nchi na nchi (intergovernmental agreement) kama uliopitishwa juzi na Azimio la Bunge siyo jambo la kigeni.
“Dosari za wazi katika mkataba huu ziondolewe, ili mkataba huu uweze kuendelea katika hatua za awali na iwapo kampuni husika tutaridhika nayo mkataba uongezwe kwa jinsi tutakavyowapima na kwa kila hatua kuzingatia maslahi ya usalama wa taifa letu,” amesema Slaa.
Alisisitiza kuwa Serikali kutafuta uwekezaji binafsi kwenye Bandari ya Dar es Salaam ni jambo jema, lakini ni vyema lifanyike kwa umakini mkubwa.
“Ninatoa tahadhari kuanzia mwanzo kuwa si nia wala lengo la taarifa hii kupinga uwekezaji wowote wenye tija, uwekezaji usio na hila,” alisisitiza.
Slaa, ambaye aliwahi kuteuliwa na Rais John Magufuli kuwa Balozi wa Tanzania nchini Sweden, amefafanua kuwa MOU au “Memorandum of Understanding” ni “makubaliano ya awali” ambayo pande mbili zinazotaka kuingia kwenye mkataba na kwa kawaida Serikali moja na nyingine zinatia saini.
“MOU hufuatiwa na mkataba unaoitwa Intergovernmental Agreement au kwa kifupi IGA. Hivyo mkataba huu tunaopigia kelele si wa kwanza kwa Serikali ya Tanzania”.
Hata hivyo alitoa mfano kuwa Tanzania imesaini jumla ya mikataba 2,829 ya uwekezaji, yaani “Bilateral Investment Treaties (BITS)”, na nchi za kigeni mbalimbali.
Kati ya mikataba hiyo ya BITS, jumla ya mikataba 2,219 inaendelea kutumika hadi sasa. Jumla ya mikataba yenye maslahi ya kibiashara ni 435 na ambayo inatumika ni 264.
“Tatizo siyo kwamba Watanzania tunapinga uwekezaji, wala kupinga mkataba wa uwekezaji. Hivyo mkiona tunapiga kelele kupinga MOU na IGA hii inayohusu DP World ni vema Watanzania wakapata uelewa,” alisema.