Umoja wa Afrika (AU), umeirejeshea Sudan uanachama wake iliyokuwa imesimamishwa kwa miezi mitatu ikisubiriwa kuunda Serikali ya mpito ya kiraia kufuatia kuondolewa madarakani kwa aliyekuwa Rais wa muda mrefu wa nchi hiyo, Omar al-Bashir.
Mwezi Agosti mwaka huu, jeshi na vyama vya kiraia pamoja na viongozi wa maandamano walitia saini mkataba wa miaka mitatu wa kugawana madaraka na kumteua Abdalla Hamdok kuwa Waziri Mkuu wa nchi hiyo.
Baada ya kuchaguliwa Hamdok aliunda baraza la mawaziri siku ya Alhamisi ambalo ni la kwanza tangu mwezi Aprili alipoondolewa madarakani Omar al – Bashir.
Makubaliano ya kuirejesha tena Sudan kwenye umoja huo wa AU yaliafikiwa katika mkutano uliofanyika mjini Addis Ababa Ethiopia ambapo baraza la amani na usalama la umoja wa Afrika lilipiga kura kuiondoa Sudan katika kizuizi cha kuwa mwanachama wa AU.
Ikumbukwe kuwa Sudan ilisimamishwa uanachama wake katika umoja wa Afrika mwezi Juni mwaka huu, kufuatia vurugu za maandamano ambapo madaktari wa upande wa upinzani walisema watu kadhaa waliuawa katika vurugu hizo kati ya Jeshi na waandamanaji.