Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni UNESCO, limekabidhi nakala 800 za madaftari ya kusajili taarifa za ukatili wa kijinsia kwa Serikali kupitia Wizara ya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wanawake na Makundi maalum.
Msaada huo, unaojulikana kama O3 plus umekabidhiwa na Shirika hilo kwa Wizara jijini Dodoma wakati wa uzinduzi wa Dawati la jinsia kwa lengo la kuhakikisha upatikanaji wa elimu bora unashirikisha wadau wa elimu kwa kuweka mazingira salama na jumuishi ya kusomea kwa wanafunzi wa taasisi za elimu ya juu na elimu ya kati wa Tanzania.
UNESCO imesema, inaunga mkono juhudi za Serikali kwenye kuanzisha na kuendesha shughuli za dawati la jinsia katika taasisi za elimu ya juu na elimu ya kati, imeshirikiana na uongozi wa chuo kikuu cha Dodoma kawenye ufunguzi wa dawati la Jinsia na kukabidhi madaftari ya usajili wa taarifa za vitendo vya ukatili wa kijinsia.
Kupitia mradi huo unaofadhiliwa na serikali ya Sweden UNESCO, jumla ya nakala 800 za madaftari ya kusajili zimechapishwa, ili kuwezesha ufuatiliaji wa mwenendo wa shauri lililopewa rufaa na kusaidia kuongeza wigo wa kupata taarifa za vitendo vya ukatili.
Kusudio jingine ni kuwezesha uandaaji wa taarifa za vitendo vya ukatili wa kijinsia zilizoripotiwa katika Dawati, ambapo UNESCO inalenga kuongeza uelewa wa wadau zaidi ya 50,000 wa vyuo vikuu kuhusu ukatili wa kijinsia na vitendo vya unyanyasaji wa kingono.
Aidha shirikia hilo pia litatoa samani kwa ofisi za madawati 10 ya jinsia ya vyuo vikuu, kutoa mafunzo kwa waratibu wa madawati ya jinsia wapatao 200 kutoka vyuo vikuu 15, na kuwezesha usambazaji wa nakala za vitabu vya rejista ya dawati la jinsia kwa vyuo vikuu vilivyoainishwa kunufaika na mradi huo.