Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania – TAFIRI, inatarajia kuanza kutumia rasmi mfumo wa kuwapatia wavuvi wadogo taarifa ya mahali samaki walipo ili wavuvi hao waweze kuvua kwa tija na kuondokana na uvuvi wa kubahatisha.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega ameyabainisha hayo jijini Dar es Salaam, mara baada ya kufungua rasmi mkutano wa siku tatu kwa ajili ya maadhimisho ya miaka 40 ya TAFIRI.

Amesema, Naibu Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Dotto Biteko anatarajia kuzindua mfumo huo Alhamisi wiki hii wakati wa kufunga mkutano huo, ambapo amesisitiza ni mfumo muhimu katika kuwawezesha wavuvi wadogo kufanya shughuli za uvuvi wakiwa na taarifa sahihi kwa kutumia simu ya mkononi.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega.

“Maana ya jambo hili ni kwamba wavuvi wanaondolewa kwenye kuwinda samaki ambapo watakuwa wanaenda kuvua samaki wakiwa na taarifa za wapi samaki walipo na umbali gani hivyo kumsaidia mvuvi kujua rasmi muda watakaotumia pamoja na kiwango cha mafuta ya boti zao.” Amesema Mhe. Ulega

Aidha ameitaka TAFIRI kuongeza vivutio vya samaki maeneo mbalimbali ya Bahari ya Hindi na maji mengine ili yavute samaki wengi kuzaliana na kuongeza uzalishaji wa samaki na kuondokana umasikini ili kuongeza kipato cha mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla kwa kuwa ni sera ya uchumi wa buluu.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa TAFIRI Dkt. Ismael Kimirei amesema taasisi hiyo iliyoanza kazi rasmi kufanya utafiti Mwaka 1983, mfumo ambao unatajia kuzinduliwa kwa ajili ya kuwapatia taarifa wavuvi kupitia simu ya mkononi ni utafiti ambao umechukua muda mrefu hadi kufikia hatua ambayo mfumo uko tayari kuanza kutumika.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Zanzibar – ZAFIRI, Zakaria Khamis amesema kuna baadhi ya tafiti wamekuwa wakifanya pamoja na TAFIRI ili kuongeza utaalamu ikiwemo ya hivi karibuni kuangalia wingi wa samaki wadogo na kwamba matokeo yake yatatoka hivi karibuni.

Taasisi zaitikia wito sitisho matumizi ya Kuni, Mkaa
Habari kuu kwenye Magazeti ya leo Oktoba 25, 2023