Taasisi ya Kuzuia  na Kupambanana Rushwa (Takukuru), imeeleza kuwa imeanza kuchunguza taarifa zilizotolewa na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi kuwa alishawishiwa kupokea rushwa ya shilingi bilioni 5 na Wafanyabiashara wawili wakubwa.

Hivi karibuni, Lukuvi aliliambia gazeti la Mwananchi lililofanya nae mahojiano maalum kuwa alikataa kiasi hicho cha fedha alichoahidiwa na wafanyabiashara hao waliotaka awasaidie kupitisha mpango wao wa kuiuzia serikali ardhi kwa mabilioni ya fedha katika eneo lililopangwa kujengwa mji mpya wa Kigamboni.

Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Valentino Mlowola jana aliwaambia waandishi wa habari kuwa Taasisi hiyo imeanza kufanyia uchunguzi taarifa hizo ikiwa ni mpango wake mpya wa kuchunguza kila taarifa za rushwa zinazotolewa.

“Kueleza tumeanza lini hilo ni suala la kiufundi, tumeshaanza kushughulikia,” Mlowola anakaririwa.

Katika maelezo yake, Waziri Lukuvi alieleza kuwa wafanyabiashara hao walinunua ardhi kutoka kwa wananchi kwa shilingi milioni 5 kwa ekari moja, lakini wakata kuiuzia serikali ardhi hiyo kwa shilingi milioni 141 kwa ekari moja tu.

“Niligundua pale kuna udanganyifu na wizi mkubwa. Haiwezekani mwekezaji anunue kutoka kwa wananchi ekari moja kwa Sh5 milioni, kisha Serikali tumlipe Sh141 milioni kwa ekari kwa kuvuka pantoni tu. Ni wizi mkubwa,” alisema Lukuvi.

Alisema kuwa wafanyabiashara hao waliwaeleza marafiki wake wa karibu kuwa wamepanga kumpa kiasi hicho cha fedha kama rushwa ili kuupitisha mpango wao lakini mpango wao ulishindikana kwake.

Rais wa Malawi apinga utabiri wa T.B Joshua kuhusi kifo chake, amuita Muongo
Mama Terry anavyoingiza Mamilioni kwa 'PhD ya Ngono'