Mfumuko wa Bei wa Taifa kwa mwaka ulioisha Januari, 2023 umeongezeka hadi asilimia 4.9 kutoka asilimia 4.8 kwa mwaka ulioishia mwezi December, 2022 ukichangiwa na kuongezeka kwa mfumuko wa bei kwa baadhi ya bidhaa za vyakula na bidhaa zisizo za vyakula
Takwimu za Ofisi ya Taifa ya Takwimu – NBS, zinaonesha kuwa kasi ya mabadiliko ya bei za bidhaa na huduma kwa mwaka ulioishia mezi January, 2023 imeongezeka ikilinganishwa na kasi iliyokuwepo kwa mwaka ulioishia mwezi December, 2022.
Baadhi ya bidhaa za vyakula zilizoonesha kuongezeka kwa Mfumuko wa bei kwa mwaka ulioishia mwezi January, 2023 ikilinganishwa na mwaka ulioishia mwezi December, 2022 ni pamoja na ngano kutoka asilimia 6.0 hadi 7.7, unga wa mtama kutoka asilimia 1.0 hadi 3.9 na samaki kutoka asilimia 4.2 hadi 4.3,
Nyingine ni matunda kutoka asilimia 1.9 hadi 5.5, mbogamboga kutoka asilimia 3.6 hadi 5.2, viazi vitamu asilimia 3.9 hadi 5.3, choroko kutoka asilimia 1.3 hadi 5.6 na kunde kutoka asilimia 8.7hadi 13.9.
Baadhi ya bidhaa zisizo za vyakula zilizoonesha kuongezeka kwa Mfumuko wa bei ni nguo za wanawake kutoka asilimia 2.6 hadi 2.7, viatu vya Wanawake asilimia 3.4 hadi 3.5 na vifaa muhimu kwa matumizi ya nyumbani asilimia 2.2 hadi 3.5.
Nyingine ni Dizeli kutoka asilimia 27.4 hadi 33.1, petroli asilimia 3.7 hadi 4.7, ada za shule asilimia 0.7 hadi 2.9 na huduma ya malazi kwenye hoteli na nyumba za kulala wageni kutoka asilimia 0.9 hadi asilimia 3.8.