Wasimamizi wa Sheria mipakani, wametakiwa kusimamia na kudhibiti gesi zinazochangia kumong’onyoa tabaka la ozoni pamoja na kuchangia ongezeko la kiwango cha joto duniani hivyo husababisha mabadiliko ya tabianchi.

Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Mazingira, Ofisi ya Makamu wa Rais, Mhandisi Catherine Bamwenzaki ametoa wito huo hii leo Februari 10, 2023 wakati akifungua mafunzo kwa maafisa wa Serikali waliopo katika mpaka wa Horohoro mkoani Tanga, kuhusu udhibiti wa uingizaji nchini wa gesi na vifaa vyenye gesi zinazomong’onyoa tabaka la ozoni.

Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Mazingira, Ofisi ya Makamu wa Rais, Mhandisi Catherine Bamwenzaki leo Februari 10, 2023akifungua mafunzo kwa maafisa wa Serikali waliopo katika mpaka wa Horohoro mkoani Tanga, kuhusu udhibiti wa uingizaji nchini wa gesi na vifaa vyenye gesi zinazomong’onyoa tabaka la ozoni.

Amesema, Wasimamizi hao pia wanatakiwa kuwaelimisha wananchi kuhusu umuhimu wa kuhifadhi tabaka la ozoni ambalo kama likimong’onyoka huruhusu mionzi zaidi ya urujuani kufikia uso wa dunia ambayo huathiri afya ya binadamu na mazingira na kuhamasisha matumizi ya gesi mbadala ambazo ni rafiki kwa afya ya binadamu na mazingira.

Bi. Catherine ameongeza kuwa, kemikali au gesi zinazotumika katika majokofu, viyoyozi, vifaa vya kuzimia moto, usafishaji chuma, utengenezaji magodoro, ufukizaji wa udongo katika vitalu vya tumbaku, kilimo cha maua na hifadhi ya nafaka katika maghala ambazo huingizwa nchini kupitia mipaka mbalimbali husababisha madhara yakiwemo saratani ya ngozi, upofu na athari kwa ukuaji wa mimea na viumbe hai wengine.

Mhandisi Catherine Bamwenzaki akiwa katika picha ya pamoja na maafisa wa Serikali waliopo katika mpaka wa Horohoro mkoani Tanga wakati wa mafunzo kuhusu udhibiti wa uingizaji nchini wa gesi na vifaa vyenye gesi zinazomong’onyoa tabaka la ozone yanayofanyika kwa siku mbili mpakani hapo.

“Serikali pia imeandaa na inatekeleza Mpango wa Kuondosha Kemikali Zinazomong’onyoa Tabaka la Ozoni Jamii ya Hydrochlorofluorocarbons (HCFCs) ifikapo mwaka 2030 na chini ya mpango huu mojawapo ya shughuli zinazotelekezwa ni pamoja na kutoa mafunzo kwa maafisa Forodha na wasimamizi wa Sheria kuhusu utekelezaji wa Kanuni za Usimamizi wa Mazingira,” amesema.

Katika mafunzo hayo, jumla ya maafisa wa serikali 720 kutoka mamlaka mbalimbali za udhibiti
wamepatiwa mafunzo na wameelimishwa kuhusu Sheria ya Usimamizi wa Mazingira (Kanuni za Kudhibiti Kemikali Zinazoharibu Tabaka la Ozoni), 2022, mada iliyowasilishwa na Mkurugenzi wa Kitengo cha Huduma za Sheria Ofisi ya Makamu wa Rais Bw. Dustan Shimbo, Sayansi ya Ozoni.

Dkt. Mollel: Bima ya Afya ni suluhu changamoto ya magonjwa
Tetemeko Syria, Uturuki: Sita wakutwa hai chini ya kifusi