Serikali nchini na Benki ya Dunia- WB zimesaini mikataba miwili ya mkopo nafuu na msaada wa dola za Kimarekani milioni 579.93 ambazo ni sawa na Sh. 1.333 Trilioni, kwa ajili ya kutekeleza miradi miwili ukiwemo wa kuboresha afya ya Mama na Mtoto na wa maji safi na usafi wa mazingira.
Mikataba hiyo, imesainiwa Jijini Dar es Salaam na Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Mwigulu Nchemba na Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Dunia, Nathan Belete ambapo kati ya fedha hizo, dola za Marekani milioni 550 sawa na shilingi za Tanzania trilioni 1.264 ni mkopo wenye masharti nafuu kutoka Benki ya Dunia na dola za Marekani milioni 29.93 sawa na shilingi bilioni 68.79 ni msaada kutoka Mfuko wa Global Financing Facility na ESMAP.
Akiongea baada ya zoezi hilo, Dkt. Nchemba amesema, “Miradi iliyopewa fedha inaendana na malengo ya Taifa ya kuboresha Maisha ya watu kupitia Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa miaka mitano 2021/2022 hadi 2025/2026, na dira ya Zanzibar ya 2050, ikiwa ni ajenda ya Serikali ya kuongeza upatikanaji wa maji vijijini na mijini na uboreshaji wa mazingira na utoaji wa huduma bora za afya na za uhakika za Mama na Mtoto, Bara na Zanzibar.”
Aidha amesema mradi wa mpango endelevu wa Maji na Usafi wa Mazingira umetengewa dola za Marekani milioni 300 sawa na Sh. bilioni 689.51 ambazo ni mkopo wenye masharti nafuu kupitia dirisha la IDA na dola milioni 4.93 ambazo ni msaada huku Mradi wa kuboresha Afya ya Mama na Mtoto ukipewa dola za Marekani milioni 250 sawa na Sh. bilioni 574.59 na msaada wa dola za Marekani milioni 25 sawa na Sh. bilioni 57.46.