Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa amesema Tanzania bado inahitaji wawekezaji na kupitia kwenye uwekezaji, inapata fursa ya mitaji na teknolojia za kisasa.

Ameyasema hayo jijini Dar es salaam wakati akizungumza na Balozi wa Tanzania nchini Canada, Alfayo Kidata ambaye alifika kumuaga.

Majaliwa amemtaka Balozi Kidata atumie fursa ya uwepo wake nchini Canada kuangalia namna ya kuisadia nchi kuimarisha sekta za kilimo, madini na utalii.

“Tukiimarisha sekta hizi, uchumi ndani ya nchi unakua lakini pia tunategemea kutumia nchi rafiki kukuza uchumi wetu wa ndani kwa maana ya kukuza mitaji na kupata teknolojia za kisasa,” amesema Majaliwa.

Amemtaka Balozi huyo akasimamie pia suala la upatikanaji wa masoko kwa ajili ya mazao yanayozalishwa nchini ili wafanyabiashara na wakulima wa Tanzania waweze kuuza bidhaa zao nje ya nchi.

Aidha, kwa upande wake Balozi Kidata amesema atahakikisha anayafanyia kazi maelekezo yote aliyopewa na Waziri Mkuu.

Hata hivyo, ameongeza kuwa anatambua kwamba Canada ina idadi ya watu zaidi ya milioni 40 na atafanya juhudi zaidi za kuitangaza Tanzania ili waje kuona vivutio vilivyopo nchini. Pia atafuatilia fursa za mafunzo kwa wanafunzi wa Kitanzania.

Video: Kupigiwa simu na mkuu wa nchi si kitu kidogo, 'nilishtuka sana'- Prof. Mkumbo
Qchillah asitisha kuacha muziki, adai haikuwa kiki