Serikali Nchini, imelitaka Shirika la Umoja wa Mataifa la kuweka usawa kwenye kuzuia, kujiandaa na kukabiliana na majanga yanayoendelea kutoka Duniani na kuziwesha nchi zinazoendelea kupata fursa sawa za uwekezaji wa viwanda vya dawa, chanjo, vifaa na vifaatiba, pamoja na misaada ya rasilimali kwenye kukabiliana na majanga.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu wakati akiwasilisha Tamko la Serikali kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwenye kikao cha Azimio la Kukabiliana na majanga na dharura kilichofanyika kwenye Mkutano Mkuu wa 78 wa Umoja wa Mataifa Jijini Newyork.
“Kama nchi moja haipo salama, basi sote hatupo salama, tunahitaji kuona mabadiliko ya usawa wa kupambana na majanga na kuwa na maazimio yenye kuleta usawa kwenye mapambano dhidi ya magonjwa ya mlipuko na dharura za masuala ya afya” amesema Waziri Ummy.
Aidha ameongeza kuwa, nchi mbalimbali ikiwemo Tanzania zimejifunza mengi kupitia mlipuko wa Ugonjwa wa UVIKO-19 na namna ulivyoleta athari ndani ya jamii, hivyo ni nyema kuwa na mikakati endelevu yenye usawa katika kukabiliana majanga.