Shirika la Ufadhili la Serikali ya Marekani limetoa uamuzi wake na kuinyima Serikali ya Tanzania Msaada wa dola 472.8, sawa na shilingi za Tanzania trilioni moja kutokana na kutoridhishwa na kufanyika kwa uchaguzi wa marudio visiwani Zanzibar pamoja na utekelezwaji wa Sheria ya Makosa ya Mtandao ya Mwaka 2015.

Uamuzi huo umetolewa kupitia Bodi ya Shirika la Changamoto za Milenia (MCC) ambayo imedai kuwa Tanzania imeshindwa kufikia viwango anavyopaswa kuwa navyo mnufaika wa msaada huo.

“Serikali ya Tanzania haijachukua hatua za kuhakikisha kuheshimiwa kwa uhuru wa kujieleza na uhuru wa kujumuika katika utekelezwaji wa Sheria ya Uhalifu wa Mtandao,” imeeleza Taarifa ya MCC.

Imeongeza kuwa Tanzania iliendelea na uchaguzi wa marudio wa Zanzibar ambao inadai haukuwa shirikishi kwa watu wote na haukuakisi maoni ya watu wote.

Ripoti hiyo imesema Tanzania haikusikiliza pia malalamiko kutoka katika Serikali ya Marekani na Jamii za Kimataifa kuhusu suala la uchaguzi wa Zanzibar.

Uchaguzi wa marudio wa Zanzibar ulifanyika Machi 20 mwaka huu kama ulivyopangwa na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC). Tume hiyo iliufuta uchaguzi uliofanyika Oktoba 25 kwa madai kuwa uligubikwa na udanganyifu.

Chama cha Wananchi (CUF), ambacho ni chama kikuu cha upinzani visiwani humo kilisusia uchaguzi wa marudio, uamuzi uliompa nafasi zaidi mgombea wa CCM, Dk. Ali Mohammed Shein kushinda kwa kishindo uchaguzi huo.

Picha: Magufuli ashtukiza tena, apata chakula kwenye Mgahawa
Yanga, Azam Kurusha Karata Zao Azam Sports Federation Cup