Serikali kupitia Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano Dhidi ya Uviko-19, imeipatia Taasisi ya Utafiti wa Kilimo – TARI, kituo cha Dakawa jumla ya Shilingi 30 milioni kwa ajili ya kusafisha mbegu za asili za zao la mpunga ili kupata mbegu bora.
Meneja wa TARI – Kituo cha Dakawa, Dkt. Jerome Mghase ameyasema hayo hivi karibuni wakati akizungumza na Maafisa Habari kutoka Idara ya Habari – MAELEZO kuhusu umuhimu wa mbegu za asili za mpunga zinazolimwa katika maeneo mbalimbali nchini.
Meneja TARI – Kituo cha Dakawa, Dkt. Jerome Mghase
Amesema, “Tunaboresha mbegu ili tuweze kupata tija na wakulima waweze kufanya kilimo chenye tija. tunazisafisha mbegu za asili za mpunga kuhakikisha tunapata mbegu bora kwani kwa sasa zilizopo zimechanganyika sana, tunatarajia kuzivuna mbegu hizi mwezi Septemba, 2023 na baada ya hapo zitaanza kufanyiwa majaribio kupitia mashamba darasa kwa wakulima ili waweze kuzielewa na kuzitumia.”
Dkt. Mghase ameongeza kuwa, mbegu za asili zinaonekana zina sifa ambazo ni muhimu katika soko pamoja na kuwa hazizai sana, pia kuna wateja ambao bado wanazihitaji mbegu hizo kwa sababu ya sifa mbalimbali, hivyo ni muhimu kuzitunza mbegu hizo kwa kuzifanyia utafiti na kuzifanya kuwa bora.
Baadhi ya mashamba yanayolimwa mbegu za zao la mpunga yaliyopo TARI – Dakawa, Morogoro
Kwa upande wake Mtafiti kutoka taasisi hiyo, Barnabas Sitta amefafanua kuwa mbegu za asili zinasafishwa ili kupata mbegu bora ambapo mpaka sasa taasisi hiyo imekusanya aina mbalimbali za mbegu zaidi ya 54 kutoka katika mikoa zaidi ya 16.
Aidha, mbegu hizo zinatumika kwa ajili ya kufanya tafiti zao kwani moja ya chanzo kinachotumika kuboresha mbegu ni kwa kupitia mbegu za asili kwa kuwa mbegu nyingi za asili ni stahimilivu katika ukame, kinzani kwa magonjwa na zina ubora wa muonekano hivyo taasisi inatumia vinasaba kutoka kwenye mbegu za asili na kutengeneza mbegu bora zaidi.
Mtafiti kutoka taasisi ya TARI, Barnabas Sitta
“Zaidi ya asilimia 70 ya wakulima wanatumia mbegu za asili katika maeneo mbalimbali hivyo kwa kuzifanyia utafiti, tunataka wakulima wapate mbegu ambazo ni safi zisizokuwa na mchanganyiko wa mbegu zingine, tunafanya hivi kwa sababu wakulima hawana mbegu rasmi ya asili hali inayopelekea kushusha ubora wa mchele”, alisema Sitta.
Kituo cha TARI Dakawa, ni miongoni mwa vituo 17 vinavyounda Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania, ina jukumu la kutafiti na kuratibu zao za mpunga kitaifa.