Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mwanaidi Ali Khamis, amewataka watendaji katika ngazi mbalimbali kuweka mkakati wa utatuzi wa kero za jamii ikiwemo ndoa za utotoni na vitendo vyote vya ukatili wa kijinsia.
Naibu Waziri Mwanaidi ametoa agizo jijini Dodoma wakati akifungua Baraza la Wafanyakazi la Wizara ya Afya-Idara ya Maendeleo ya Jamii liliofanyika katika ukumbi wa Makao ya Taifa ya Watoto ya Kikombo.
Amesema kuwa Wizara inatakiwa kuwatumia ipasavyo watumishi wake katika kuhakikisha mipango iliyowekwa inasimamiwa na kutekelezwa kikamilifu ili kuboresha huduma za Wizara hiyo na kutatua changamoto mbalimbali katika jamii.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu Wizara ya Afya-Idara ya Maendeleo ya Jamii Dk. John Jingu, amesema lengo la Baraza hilo la Wafanyakazi ni kushirikiana watumishi katika mipango na utekelezaji wa majukumu ya wizara.