Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania ( TAWA) imetekeleza kwa vitendo maagizo yaliyotolewa Desemba mosi, 2022 na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Maadhimisho ya kitaifa ya Siku ya Ukimwi duniani yaliyofanyika Mkoani Lindi ya kuhakikisha kuwa madhara yaletwayo na wanyama wakali na waharibifu yanadhibitiwa.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Maliasili na Utalii, Juma Mkomi amesema, zoezi hili la kuwavalisha tembo visukuma mawimbi litasaidia kuondoa madhara yaletwayo na wanyama hao kwani vifaa hivyo vinafuatilia mienendo ya tembo na vitawaongoza askari katika zoezi la kuwarudisha hifadhini kabla hawajafika katika makazi ya wananchi.
Awali, Kaimu Naibu Kamishna wa Uhifadhi, Mlage Kabange akizungumza kwa niaba ya Kamishna wa Uhifadhi TAWA, alisema wametoa mafunzo ya kijeshi kwa vijana wanaoishi pembezoni mwa hifadhi ‘Village Game Scouts (VGS),’ watakaotumika kama Askari wa Akiba katika kukabiliana na changamoto ya wanyama hawa hususan katika vijiji ambavyo matukio ya kuvamiwa na tembo yamekuwa yakijirudia.
Aidha, TAWA pia imenunua pikipiki zilizofungwa vifaa maalumu vya kutoa matangazo kwa wananchi zitakazotumika katika maeneo ambayo magari ya doria hayawezi kuyafikia ambapo Naibu Kamishna Kabange aliongeza kuwa TAWA imekamilisha ujenzi wa nyumba za askari ambazo zimejengwa katika vijiji vya Nditi na Ngumbu vilivyopo katika wilaya za Nachingwea na Liwale.
Vijiji hivi vimekuwa vikipata changamoto kubwa ya wanyama wakali na waharibifu na TAWA imekuwa ikishirikiana na Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori Tanzania (TAWIRI), kwenye zoezi hilo la ufungaji wa visukuma mawimbi na la kurudisha makundi ya tembo kutoka vijiji vilivyopo Mkoani Lindi na kuwarudisha hifadhini.