Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA), imeyaruhusu makampuni ya ndege za Kenya yaliyokuwa yamefungiwa kuendelea kufanya shughuli zake nchini baada ya Kenya kuondoa zuio la Watanzania wanaoenda Kenya, kuwekwa karantini.
Taarifa hiyo imetolewa leo Septemba 16, 2020, na Mkurugenzi Mkuu wa TCAA Hamza Johari, ambaye amesema kuwa tamko hilo linakuja baada baada ya Serikali ya Kenya kuiondolea Tanzania vikwazo vya raia wake kuingia nchini humo bila kuwekwa karantini.
Aidha ameyataja mashirika ya Ndege za Kenya yaliyoruhusiwa kuendelea na shughuli zake kuwa ni Kenya Airways, Fly 540 Limited, Safarilink Aviation na AirKenya Express Limited.
Septemba 15, 2020, nchi ya Kenya ilitoa orodha ya nchi 147 ambazo raia wake wataingia nchini humo bila kuwekwa karantini na katika nchi hizo mojawapo ni Tanzania.