Siku mbili kabla ya mtanange kati ya Young Africans SC na TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia na Maendeleo (DRC), Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limesema kuwa limepokea taarifa kuwa ‘Wana Jangawani’ wamepanga kufanya vurugu katika mchezo huo.

Taarifa ya TFF kwa vyombo vya habari imeeleza kuwa imeeleza kuwa wamefahamishwa mpango wa baadhi ya viongozi wa Young Africans SC kuwashawishi mashabiki wao kufanya vurugu dhidi ya warushaji matangazo ya televisheni ya moja kwa moja wakati wa mchezo wa Kombe la Shirikisho la Afrika ngazi ya Makundi, utakaofanyika Juni 28 mwaka huu.

Shirikisho hillo limewataka viongozi hao kuacha mara moja mpango huo kwani ni kinyume na kanuni za mashindano na mikataba ya udhamini katika hatua hii.

“Ikumbukwe kwamba CAF inamiliki asilimia mia moja ya haki za habari na masoko katika ngazi hii ya makundi na jaribio lolote la kukwamisha matangazo ya biashara au utengenezaji na urushaji wa matangazo ya televisheni au ukwamishaji wa shughuli zingine kama hizo kwa CAF au wakala aliyeteuliwa na CAF kutaigharimu klabu mwenyeji si kwa kutozwa faini tu lakini pia uwezekano wa kuondolewa mashindanoni,” imeeleza sehemu ya taarifa hiyo.

TFF pia imetahadharisha kuhusu utamaduni wa kukaa uwanjani ili kuepusha aina yoyote ya vurugu kwenye michezo yake hususani hii ya hatua ya makundi.

“Wapenzi wa Yanga wanaombwa kufika kwa wingi na kuishangilia kwa nguvu  timu yao ikiwa ni njia ya kuitia hamasa.Hata hivyo shamrashamra hizo zifanyike kwa kufuata sheria,kanuni na taratibu za Mpira wa Miguu na sheria za nchi,” imesema TFF kupitia taarifa yake hiyo.

Mtanange kati ya Young Africans na TP Mazembe utashuhudiwa Juni 28, 2016 saa 10.00 jioni kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Magufuli apangua safu wakuu wa wilaya, Mkoa... Polepole akabidhiwa Ubungo, Mulongo 'nje'
Euro2016: Poland yailaza Switzerland