Wakati Michuano ya Kombe la Shirikisho la Azam yaani Azam Sports Federation Cup (ASFC), ikiwa imeanza jana Novemba 02, 2017 na kuendelea leo Ijumaa na kesho Jumamosi, Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), limetoa ufafanuzi wa malipo kwa hatua hii ya awali.
Kwa hatua za awali na hatua ya kwanza, TFF imetoa ufafanuzi kwamba kwa timu mwenyeji inalipwa shilingi lakini saba na elfu hamsini (Sh. 750,000) wakati timu ngeni inayosafiri hadi kituo cha mchezo inalipwa shilingi milioni mbili na lakini tano (Sh 2.5m). Fedha zote hizo, zinalipwa katika akaunti ya kila timu.
Lakini TFF imetoa ufafanuzi kwamba, kwa timu ambazo zinatoka katika kituo kimoja (mkoa mmoja) zote zitalipwa Sh 750,000 kama gharama sawa licha ya moja ya timu itakuwa mgeni na nyingine mwenyeji.
TFF imetoa ufafanuzi huo, baada ya kuibuka mjadala wa dhana ya uenyeji na ugeni licha ya kwamba timu shindani zinatoka kituo kimoja (mkoa mmoja). Timu hizo zielewe kwamba zitalipwa gharama inayofanana katika maandalizi.
Fedha zitaongezeka kwa timu ambayo inasonga mbele baada ya hatua ya awali na hatua ya kwanza.
Katika hatua nyingine, TFF inasubiri taarifa za Kamishna na Mwamuzi kuhusu vurugu zinazodaiwa kutokea huko Simiyu katika mchezo kati ya Usalama na Sahare All Stars uliofanyika Novemba 2, mwaka huu.
TFF imepanga mchezo kati ya Kisarawe United ya Pwani na Silabu ya Mtwara ufanyike kesho Novemba 4, mwkaa huu baada ya kuahirishwa Novemba 2, mwaka huu baada ya wachezaji wake kupata ajali maeneo ya Mchinga mkoani Lindi wakiwa safarini kwenda Pwani. Mechi inayofanyika leo Novemba 3, mwaka huu kati ya Buseresere ya Geita itayocheza na Isako ya Songwe.
Baada ya mechi hizo,itakuja Raundi ya Kwanza ya ASFC ambayo itachezwa ama Novemba 7, 8 au 9 ambako TFF imepanga kesho kutuma fedha zote za maandalizi ya timu husika ili kusiwe na kisingizio chochote cha kujiandaa.
Kaimu Katibu Mkuu wa TFF, Kidao Wilfred ameagiza Idara ya Fedha na Utawala ya TFF kulipa fedha kwa timu hizo haraka, lakini kwenye akaunti ya timu husika badala ya mwakilishi ye yote au kiongozi.
Timu ambayo haijafungua akaunti watakuta fedha hizo kwenye Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa (FA), lakini TFF ingependa kusisitiza kwa wadau hao kufufua akaunti au kufungua akaunti haraka.
Katika raundi hiyo ya kwanza Mashujaa ya Kigoma itacheza na Mshindi kati ya Buseresere ya Geita na Isako ya Songwe; wakati mechi nyingine zitakuwa Msange ya Tabora itacheza na Milambo pia ya Tabora ilihali Bulyanhulu ya Shinyanga itacheza na Area C ya Dodoma.
Kwa mujibu wa droo, Mji Mkuu FC ya Dodoma imeangukia kwa Nyundo ya Kigoma wakati Baruti FC ya Mara itacheza na Ambassodor ya Kahama, Shinyanga huku Eleven Stars ya Kagera ikipangwa kucheza na Ndovu ya Mwanza.
Changanyikeni ya Dar es Salaam itacheza na Reha FC pia ya Dar es Salaam wakati Mshindi kati ya Kisarawe United na Silabu ya Mtwara atacheza na Kariakoo ya Lindi huku Cosmopolitan ikicheza na Ajabalo wakati Makumba FC itapambana na Green Warriors ya Kinondoni wakati Namungo FC ya Lindi itachuana na Villa Squad ya Dar es Salaam huku Dar City ikicheza na Majimaji Rangers ua Nachingwea.
Michezo mingine ya hatua ya kwanza itakutanisha timu za Shupavu FC ya Morogoro na Sabasaba pia ya mjini humo wakati Motochini FC ya Katavi dhidi ya Ihefu FC ya Mbeya wakati The Mighty Elephant ya itacheza na Makanyagio ya Rukwa.
Timu ya Burkina FC ya Morogoro itacheza na Mbinga United ya Ruvuma wakati Makambako Heroes ya Njombe itacheza na Mkamba Rangers ya Morogoro wakati Real Moja Moja itapambana na African Wonderers – zote za Iringa. Boma FC ya Mbeya itacheza na African Sports ya Tanga.
Mechi nyingine za hatua hiyo itakuwa ni kati ya Pepsi ya Arusha ambayo itacheza na Kilimanjaro Heroes ya Kilimanjaro; huku Stand Misuna ya Singida itacheza na Madini FC ya Arusha ilihali AFC ya Arusha itacheza na Nyanza ya Manyara wakati New Generation itacheza na Mshindi kati ya Usamala FC na Sahale ya Tanga. Bodaboda FC itacheza na Kitayose ya Kilimanjaro.
Michuano hiyo ambayo Bingwa Mtetezi ni Simba SC ya Dar es Salaam, inashirikisha timu 91 msimu huu kwa mchanganuo wa timu 16 za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL); 24 za Ligi Daraja la Kwanza (FDL); 24 za Ligi Daraja la Pili (SDL) na 27 za Ligi ya Mabingwa wa Mkoa (RCL).