Baada ya kutangazwa kuachwa na  ‘Wagonga nyundo’ wa jiji la Mbeya, Mbeya City mshambuliaji Themi Felix ‘Mnyama’ ameibukia kwa wakata miwa wa Kagera Sugar na muda wowote kuanzia sasa atasaini kandarasi na wanankulukumbi hao ambao tayari wameshamalizana na Edward Christopher.

Themi aliwahi kuwa mshambuliaji tishio miaka mitatu iliyopita akiwa na Kagera kabla ya kuhamia City ambapo kiwango kilishuka na sasa anategemea kurudi nyumbani kuendelea kufanya mambo makubwa.

Wachezaji wengine ambao wameshamwaga wino kuwatumikia wakata miwa hao ni David Burhan, Matogolo Anthony na Hassani Khateeb.

Mratibu wa Kagera Sugar, Mohamed Hussein alizungumzana Dar24.com na kusema uongozi wa klabu hiyo umeamua kusajili wachezaji wenye uzoefu mkubwa wa ligi ili iwe rahisi kurejesha makali ambayo msimu uliopita hayakuonekana kabisa.

“Usajili tunafanya kwa umakini mkubwa kwa kuangalia sehemu zenye mapungufu ndani ya kikosi, tunajipanga kuleta ushindani wa kweli kwenye ligi,” Alisema Mohamed Hussein.

Kagera Sugar 1

Kagera wanatarajia kutumia uwanja wao wa Kaitaba baada ya kukamilika kwa asilimia kubwa matengenezo yake ikiwemo uwekaji wa nyasi bandia.

Msimu uliopita Wanankulukumbi walitumia uwanja wa Kambarage mkoani Shinyanga kama uwanja wa nyumbani baada ya dimba lao la Kaitaba kuwa katika matengenezo.

Manchester City Wakamilisha Usajili Wa Nolito
Hofu ya Kushambuliwa na Wazawa Yaibuka Kenya.