Mawaziri waandamizi wa serikali ya waziri mkuu wa Uingereza, Theresa May wamepanga kumshinikiza kiongozi huyo kujiuzulu, gazeti la Sunday Times la nchini humo limeripoti habari hiyo.
May anakabiliwa na kitisho cha shinikizo la kuachia wadhifa wa waziri mkuu kutokana na kusuasua kwa mkakati wake kuhusu Uingereza kujiondoa kutoka Umoja wa Ulaya, Brexit baada ya makubaliano yake na Umoja wa Ulaya kukataliwa mara mbili na bunge la nchi hiyo.
Gazeti la Sunday Times limewanukuu mawaziri 11 ambao hawakutajwa majina wakisema wamekubaliana kuwa May anapaswa kuondoka madarakani kwa sababu amegeuka kuwa kiongozi asiyetabirika na asiyeweza kuamua.
Aidha, taarifa hiyo imesema kuwa mawaziri hao wamepanga kuanza vuguvugu hilo la kumtaka May kujiuzulu siku ya Jumatatu ijayo na iwapo atashindwa wamepanga kutishia kujiuzulu.
Hata hivyo, Ofisi ya waziri ya mkuu iliyopo mtaa wa Downing haijatoa taarifa yoyote kuhusiana na ripoti hiyo ya gazeti la Sunday Times.